Kombe la UEFA
20 Februari 2008Klabu za dimba za Ujerumani,Uingereza na za Spain ,zaonesha zitaendelea kutamba leo katika kombe la Ulaya la UEFA:
Inatazamiwsa lakini, alao timu 1 katika ya 11 za nchi hizo 3, itaanguka pale Atletic Madrid itakapoumana na Bolton Wanderers ya Uingereza.
Ikiwa kila kitu kitaenda sawa, Ujerumani itaingiza timu 5 katika duru ijayo ya timu 16 za kombe hili la UEFA –miongoni mwazo- mabingwa mara kadhaa wa Ujerumani-Bayern Munich.
Leo pia uamuzi unakatwa : wapi michezo ya kwanza kabisa ya Olimpik kwa chipukizi itafanyika na Singapore inataka kutoroka na tiketi hiyo ya kuandika historia.
Ujerumani ikiwa kila kitu jioni ya leo kitaiendea sawa, itakua na timu 5 katika duru ijayo ya timu 16 za Kombe hili la UEFA.Viongozi wa Ligi-Bayern Munich yamkinika sana ikacheza leo na Aberdeen ya Scotland bila stadi wake wa Ufaransa, Franck Ribery alieumia lakini baada ya kutoka sare 2-2 huko Scotland, Munich yatazamiwa kutamba nyumbani na hasa ikicheza na jogoo lao la Itali-Luca Toni.Toni alipachika mabao 3 pekee jumapili iliopita pale Munich ilipokutana na Hannover katika changamoto za Bundesliga.
Werder Bremen iliopo nafasi ya pili nyuma ya Munich katika ngazi ya Bundesliga imefunga safari ya Ureno kukumbana huko na Braga ikiwa na mabao 3 kikapuni.Bremen inabidi lakini kucheza leo bila ya stadi wake Aaron Hunt na mbrazil Diego.
Hamburg ina matarajio pia ya kusonga mbele na kuiacha nyuma FC Zurich na hasa baada ya ushindi wao wa mabao 3-1 huko Uswisi.Bayer Leverkusen inapimana nguvu na Galatasary ya Uturuki kufuatia suluhu yao ya 0:0 mjini Istanbul.
Klabu ya 5 ya Ujerumani-Nuremberg ndio pekee yenye kasoro baada ya kuzabwa bao 1:0 na Benefica Lisbon ya Ureno duru iliopita.Kocha wao mpya Thomas van Heesen, anadai lakini timu yake bado ina nafasi ya kutamba mbele ya wareno.
Matumaini pekee ya wataliana katika kombe hili la UEFA –Fiorentina wana bao 1 mfukoni walilopachika huko Norway walipocheza na wenyeji wao Rosenborg Trondheim wakati PSV Eindhoven ,timu pekee ya Holland mashindanoni, imefunga safari ya Sweden kuonana na Helsingborg.
Atletico Madrid ya Spain iko nyuma kwa bao 1 iliozabwa na El Hadji Diouf na inakusudia kusawazisha.
Timu nyengine 2 za uingereza katika changamoto hizi-Tottenham Hotspurs na Everton ziko nafasi nzuri zaidi kuliko Bolton wanderes ya El Hadji Diouf, kusona mbele:
Tottenham-mabingwa mara 2 wa kombe hili waliowalaza wacheki Slavia Prague 2-1 watasonga mbele tu.Everton waliishinda Brann Bergen mabao 2 duru ya kwanza hawana shaka watatamba tena kwa wan orway hao.
Nje ya dimba, wakuu wa Olimpik wa China wametetea msimamo wa nchi yao china kuelekea mzozo wa dafur, huko Sudan na wametoa mwito kwa wakereketwa wa Dafur jana kuacha kuwashinikiza wafadhili kujitoa kutoka michezo ya olimpik ya Beijing majira haya ya kiangazi.
Wakereketwa wanataka serikali ya China kuitia shindo Sudan kukomesha mapigano katika mkoa wake wa dafur.
Singapore,inatumai kutoroka leo na tiketi ya kwanza kabisa ya kuandaa michezo ya vijana ya Olimpik-ikiwa ya kwanza kabisa.Rais wa Halmashauri kuu ya olimpik Ulimwenguni,mbelgiji Jacques Rogge,atazamiwa kumtangaza mshindi leo kati ya Singapore na Moscow huko Luasanne, mako makuu ya IOC-Halmashauri kuu ya olimpik ulimwenguni.