Korea Kaskazini yatakiwa iheshimu ahadi ya kukifunga kinu cha Yongbyon
22 Desemba 2007Maafisa wa Korea Kusini na Marekani wamesema leo kwamba mtaalamu wa Korea kutoka wizara ya mambo ya ndani ya Marekani, Sung Kim, amerejea mjini Seoul, Korea Kusini baada ya kuchunguza kazi ya kukifunga kinu cha nyuklia cha Yongbyon nchini Korea Kaskzini. Sung Kim alifanya ziara ya siku tatu nchini Korea Kaskazini.
Wakati haya yakirifiwa, waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice ameishawishi Korea Kaskazini itimize ahadi yake ya kuvifunga vinu yake vyote vya nyuklia.
Kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Washington hapo jana Condoleezza Rice aliitaka serikali ya Pyongyang itoe maelezo kamili kuhusu mpango wake wa nyuklia kufikia mwisho wa mwaka huu. Kiongozi huyo anatumai Korea Kaskazini itaheshimu muda huo lakini akasisitiza maelezo yanatakiwa yafanywe kwa njia iliyo sawa.
Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa kwenye mazungumzo ya mataifa sita mjini Beijing China, Korea Kaskazini ilikubali kukifunga kinu chake cha Yongbyon na kutoa maelezo kamili kuhusu mpango wake wa nyuklia kufikia mwisho wa mwaka huu.