1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea ya kaskazini itaomba radhi kwa K.kusini ?

25 Mei 2010

Mafuta yatavuja hadi lini huko Ghuba la Mexico ?

https://p.dw.com/p/NWJE
Rais Lee Myung-bak wa K.kusini, (kulia. )Picha: AP

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani,leo yamechambua mada mbali mbali tangu za ndani mfano wa juhudi za kuunda serikali ya muungano katika mkoa huu wa Northrhein- westphalia baada ya uchaguzi wa mapema mwezi huu,uchafuzi wa mazingira kwa kuvuja mafuta katika Ghuba la Mexico na mvutano mpya kati ya Korea mbili-kaskazini na kusini.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung juu ya hatua iliotangaza Korea ya Kusini ,laandika:

"Rais wa Korea ya Kusini, anadai Korea ya kaskazini iombe radhi kwa hujuma iliofanyiwa manuwari ya Korea ya Kusini , ambayo ilisababisha vifo vya wanamaji wake 46.Kutimizwa dai hilo, itakua taabu sana.Hatahivyo, dai hilo limestahiki kutolewa.

Utawala ambao unahalalisha kudumu kwake kwa kumuabudu Kiongozi wake kama Mungu-Mtu,hauwezi kuungama makosa yake, Seuze kufika umbali kutaka radhi tena hadharani.

Kwani, kutofanya hivyo ni msingi unaosimamia utawala huo.Korea ya Kusini kwahibvyo, isitumai kwamba dai lake la kuombwa radhi litaitikiwa..."

Ama gazeti la LEIPZIGER VOLKSZEITUNG kuhusu mzozo ulioibuka Korea, laandika kwamba, kinyume na debe unaojipigia utawala wa huko kuwa , umeungana na unazungumza kwa sauti moja , si kweli.Kuzeeka na kuugua Kiongozi wake Kim Jong II, kunazuisha kinyan'ganyiro cha madaraka. Gazeti laongeza:

"Mtindo wa kumuabudu Kiongozi na kurithishana uongozi kama katika ufalme,kunampa urithi ,mwana wa kiume wa Kim- Jong-un.

Lakini , mabadiliko hayo yanayokaribia ya uongozi yamezusha kinyan'ganyiro cha madaraka kati ya wanajeshi wanaopingana.Atakaeshinda kinyan'ganyiro hicho ni yule atakaetunisha misuli kwa nguvu zaidi.

Na Kim, anaelewa kwamba bila ya kuwapo kitisho kutoka nje ,utawala huo hauwezi kusimama wima.Kwa jicho hilo, jibu la Korea ya Kusini na mshirika wake Marekani juu ya tokeo baya kabisa tangu kumalizika kwa vita vya Korea 1953,halioonekani ni udhia mkubwa."

Gazeti la Ditmarscherzeitung, linazungumzia uchafuzi wa bahari kwa kuvuja mafuta katika pwani ya Marekani.Gazeti laandika:

"Kukasirika na kufadhahika hakutoshi.Rais Obama anapaswa hivi sasa kuchukua hatua tena haraka na kwa shabaha maalumu.Hafai tena kutegemea tu habari na ahadi za Kampuni la mafuta ya petroli.Kwani, ni jukumu la serikali mjini Washington, kuidhibiti hali ya mambo na kuchukua hatua haraka kuwalinda wakaazi na mazingira.

Endapo rais ataendelea kusitasita, atapoteza imani ya serikali yake kwani atajikuta anaonekana ni yuko chungu kimoja na makampuni hayo makubwa ya mafuta."

Likiendeleza mbele mada hii, gazeti la MÄRKISCHE ALLGEMEINE kutoka Potsdam, laandika:

"Tangu zaidi ya mwezi mmoja sasa, mafuta ya petroli yanavuja kwa wingi mno kutoka kisima cha mafuta katika pwani ya Marekani.Na hakuna ajuwae wala kampuni kubwa la petropli la BP,mmiliki wa Jukwaa la kuchimba mafuta lililozama,nini la kufanya kurekebisha mambo.Na hii ni dunia ambayo tunajionea kiwanda cha magari kinabidi kuyarejesha maalfu ya magari yake viwandani ili kurekebisha hitilafu,lakini yasikitisha kuwa , hakuna kikosi maalumu cha kupambana na balaa kama hilo.Cha kuhuzunisha zaidi ni kuona, katika majukwaa mengine ya kuchimba mafuta ambayo si ya kuaminika zaidi kama hili lililovuja,bado uchimbaj mafuta unaendelea bukheri-mustarehe na haukusimamishwa ili kufanya ukaguzi iwapo pia kila kitu ni salama..."

Mwandishi: Ramadhan Ali/DPA

Uhariri: Abdul-Rahman