Korea ya Kaskazini kuwekewa vikwazo zaidi?
11 Juni 2009NEW YORK.
Nchi za magharibi zimekubaliana na madola muhimu yanayoiunga mkono Korea ya Kaskazini juu ya kuiwekea nchi hiyo ya kikomunisti vikwazo zaidi katika sekta za silaha na fedha. Nchi hizo pia zimekubaliana juu ya uwezekano wa kuzikagua meli za Korea ya Kaskazini.
Hatahivyo mswada wa azimio la Umoja wa Mataifa juu ya vikwazo hivyo unapaswa kuidhinishwa na Baraza la Usalama.
Lengo la azimio hilo ni kuizuia Korea ya Kaskazini kupata na kuuza nyenzo na tekinolojia ya kuunda silaha za nyuklia na makombora ya masafa marefu.
Azimio hilo pia litawezesha kuizuia Korea ya Kaskazini kupata fedha za kugharamia mipango yake ya silaha.
Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Susan Rice amewasilisha mswada wa azimio hilo kwenye Baraza la Usalama ,ambao amesema kuwa ni jibu la kufaa ,kufuatia jaribio la pili la silaha za nyuklia lililofanywa na Korea ya Kaskazini.