Mzozo wa wakimbizi waitikisa Serikali
8 Februari 2016Tuanzie na uchukozi wa Korea ya kaskazini.Gazeti la "Flensburger Tageblatt "linaandika:"Kwa mara nyengine tena Korea ya Kaskazini imepuuza onyo la ikulu ya Marekani na jumuia ya kimataifa-hali ambayo kwa upande mwengine inalijiongeza mbele suala la madhara na kuaminika serikali ya rais Barack Obama na washirika wake.Tukiweka kando laana kutoka Umoja wa mataifa,laana ambazo Pyongyang tangu muda mrefu sasa haziwashughulishi,kuna hatua mbili zinazoweza kuzingatiwa:Kutozwa faini au kufungwa akonti za benki kubwa kubwa,japo kama ni kidogo,zinazoendesha biashara pamoja na Korea ya Kaskazini.Na kutegwa mtambo wa kinga dhidi ya makombora kwa msaada wa Marekani,katika ardhi ya Korea ya Kusini.Pindi China ikikataa kuchangia katika shinikizo hilo,basi nayo pia itabidi izidi kushinikizwa.Kwasababu mara nyingi inaonekana kana kwamba Beijing wanafuata mchezo wa ndumilakuwili:Kwa upande mmoja wanaionya Korea ya Kaskazini kwa upande wa pili lakini viongozi wa mjini Peking wanaonekana kujigeuza "ngao"kuikinga Korea ya Kaskazini.
Serikali ya shirikisho inazidi kupoteza imani ya wapiga kura
Mzozo wa wakimbizi unaendelea kugonga vichwa vya habari humu nchini.Gazeti la "Nordwest-Zeitung" la mjini Oldenburg linamulika mvutano ulioripuka ndani ya serikali kuu ya muungano kuhusiana na suala la lini familia za wakimbizi ziruhusiwe kuletwa humu nchini.Gazeti linaendelea kuandika:"Ikiwa makamo kansela,anasema mwenyewe hajui alichokipigia kura katika kikao cha mawaziri,hapo hata imani ndogo iliyokuwa imesalia kuhusiana na uwezo wa serikali hii ya muungano inatoweka.Kwa wiki sasa kansela haonekani,anajaribu bila ya mafanikio kuifanyia merekebisho sera yake iliyofeli kuhusu wakimbizi.Serikali inaonyesha imepwaya.Kwamba mpango usiofaa wa kukabiliana na mzozo unadhihirika kama chachu kwa wafuasi wa siasa kali wa vuguvugu la Pegida,hakuna anaeweza kubisha."
Kitisho cha dharuba kali chasababisha kusitishwa sherehe za Karnavali ya Jumatatu ya mawardi
Mada yetu ya mwisho magazetini inahusiana na shamra shamra za Karnaval.Kitisho cha kuzuka dharuba kali wakati wa kilele cha Chanmra shamra hizo hii leo-suiku inayojulikana kama "Jumatatu ya Mawardi" kimepelekea baadhi ya sherehe hizo kusitishwa katika baadhi ya miji ikiwa ni pamoja na Düseldorff na Mainz.Katika jiji la Cologne,waandalizi wamechukua hatua za tahadhari lakini sherehe zinaendelea kama ilivyopangwa.Gazeti la "Rheinpfalz" linaandika:"Haijawahi hata mara moja kuzungumziwa sana kuhusu usalama na kuwepo idadi kubwa ya polisi katika sherehe za Jumatatu ya Mawardi kama mwaka huu.Kila mmoja yuko katika hali ya tahadhari kuanzia wanakarnaval,maafisa wa serikali wanasiasa wanaojiandaa kwa uchaguzi dhidi ya hatari ya kutokea mashambulio ya kigaidi au makundi ya wahalifu yanayowadhalilisha wanawake.Halafu kuna kitisho cha hali ya hewa kinachotishia kufuja sherehe za Jumatatu ya Mawardi.Kiroja hiki mtu anaweza kusema.Ni jambo la kusikitisha kwa wote wale wanaohusika na maandalizi ya karnaval katika jiji la Mainz ambao kwa wiki kadhaa wamekuwa wakijiandaa na pia kwa mashabiki waliojitayarisha kusherehekea.Ni vyema kwamba Mainz wametumia busara na sio vichekesho.Ni sawa kabisa kufutilia mbali sherehe hizo kwa kutilia maanani kitisho cha dharuba kali."
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman