1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea yaelekea wapi ?

26 Mei 2010

Ziara ya bibi Hillary Clinton mjini Seoul

https://p.dw.com/p/NXNA
Hillary Rodham Clinton(kushoto) na Rais Hu Jintao (China)Picha: AP

Katika mvutano kati ya Korea mbili-Kusini na kaskazini, Korea ya kaskazini imetishia kukifunga kiungo cha mwisho cha barabara kati ya nchi hizo mbili zilizogawika.Korea ya Kaskazini imetishia kufanya hivyo iwapo Korea ya Kusini, ikiendelea na kile ilichokiita "chokochoko zake za matangazo ya Radio " yanayohanikiza upande wapili wa eneo la mpakani linalokatazwa harakati za kijeshi. Waziri wa nje wa Marekani, Bibi Hillary Clinton, aliezuru Seoul, Korea ya kusini , hivi punde ameitaka China, mshirika wa chanda na pete wa Korea ya Kaskazini, kubadili mkondo wa siasa zake.

UADUI KATI YA SEOUL NA PYONGYANG

Uhasama unaozidi kati ya ndugu hawa wawili wa Korea, umewastusha hata wawekezaji wakiwa na wasi wasi kwa umbali gani, Korea mbili zitafika katika uhasama wao. Hii inafuatia Korea ya Kusini, kuituhumu Korea ya Kaskazini , kuizamisha kwa kombora manuwari yake.

Siku moja baada ya kutangaza itakata mafungamano yote yaliiopo na Korea ya kusini, Pyongyang, imearifu sasa inazingatia kuifunga njia pekee iliosalia wazi na Korea ya Kusini,hatua ambayo ingehatarisha uzalishaji bidhaa katika Bustani yao ya pamoja ya viwanda inayoipatia mapato nono Korea ya Kaskazini.

MSIMAMO WA MAREKANI:

Marekani, iliomtuma waziri wake wa nje Bibi Hillary Clinton, hadi Korea kusini, inajaribu kuzuwia mvutano huu kati ya Korea mbili haumalizikii vitani .

Bibi Hillary Clinton, alisema akiwa mjini Seoul,

"Huu ni uchokozi wa Korea ya Kaskazini usiokubalika na Jumuiya ya Kimataifa ina wajibu wa kutoa jibu lake."

Hivyo, Bibi Clinton, ameitaka China, kumshawishi mshirika wake wa chanda na pete "amtulize shetani" na kubadili mkondo inaofuata.

"Korea ya Kaskazini bado yaweza kuchagua njia nyengine ya kufuata . Badala ya kutengwa, ufukara, vita na laana, Korea ya Kaskazini yaweza ikajumuika na nchi nyengine, ikawa na neema, amani na heshima-"

alisema bibi Hillary Clinton.

NA CHINA JE ?:

China, ambayo ndio uti wa mgongo kwa jirani yake Korea ya Kaskazini, kwa mara nyengine imetaka pawepo utulivu na mazungumzo ya pande mbili. China, imekataa kuunga mkono uchunguzi wa kimataifa uliogundua wiki iliopita, kuwa Korea ya Kaskazini, iliizamisha manuwari ya Korea ya Kusini na kuwaua wanamaji wake 46.

Kuna uhakikika kwamba, China, itatia mguu wake kuzuwia mshirika wake kuwekewa vikwzo vipya , jambo ambalo litaifanya Marekani kuridhia si zaidi ya maneno makali dhidi ya Pyongyang.

HILLARY CLINTON:

Hapo awali, bibi Hillary Clinton, alisema kuwa,mzozo ulioibuka kutokana na hatua ya Korea ya Kaskazini kuizamisha manuwari ya Kusini, unahitaji jibu kali, na kwamba Marekani, ikizingatia njia zaidi nyenginezo kuiwajibisha Korea ya kaskazini.

Licha ya tangazo lake kwamba, inakata mafungamano yote na Kusini, Korea ya Kaskazini leo, imewaachia wafanyakazi kutoka upande wa pili wa mpaka kwenda makazini mwao katikla bustani ya viwanda -mali ya nchi hizo mbili.

Mwandishi: Ramadhan Ali/ RTRE

Uhariri:Miraji Othman