Kundi la waasi Myanmar ladai kukamata kamandi ya jeshi
21 Desemba 2024Taarifa ya kundi hilo la Arakan Army (AA) imesema imechukua udhibiti kamili wa kamandi ya jeshi kwenye mji wa Ann magharibi mwa nchi hiyo jana Ijumaa, baada ya wiki kadhaa za mapigano makali. Kamandi ya Ann itakuwa ya pili kuangukia mikononi mwa waasi hao katika kipindi cha miezi mitano.
Jeshi la Myanmar linazo kamandi 14 kote nchini na nyingi kati ya hizo zinapambana hivi sasa kuyakabili makundi ya waasi ya kikabila au lile la "People's Defence Forces” lililoibuka kwa lengo la kuupinga utawala wa kijeshi ulionyakua madaraka kwa njia ya Mapinduzi mnamo mwaka 2021.
Mapigano yanalitikisa jimbo la Rakhine tangu kundi la AA lilipovishambulia vikosi vya Jeshi la Taifa Novemba mwaka jana na kuhitimisha usitishwaji mapigano ulioshuhudiwa tangu kutokea mapinduzi.