1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kura zaendelea kuhesabiwa Kenya

5 Machi 2013

Matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika jana nchini Kenya yanaendelea kutolewa huku Uhuru Kenyatta akiongoza kwa takriban ailimia 55 dhidi ya mpinzani wake Raila Odinga akiwa na asilimia 40

https://p.dw.com/p/17qR9
Uchaguzi Kenya
Uchaguzi KenyaPicha: DW/Alfred Kiti

Matokeo hayo yanayopokewa katika kituo cha kukusanyia matokeo cha Bomas mjini Nairobi yanamuonesha mgombea urais wa chama cha The National Alliance Uhuru Kenyatta akiongoza kwa kura millioni 1,507,854 dhidi ya mpinzani wake Raila Odinga wa chama cha Orange Democratic Movement aliye na kura 1, 148, 836 ya jumla ya kura zote zilizohesabiwa kufikia sasa.

Chama cha ODM tayari kimeelezea wasiwasi wake kwamba matokeo hayo si sahihi na kutilia shaka mfumo mzima wa uwasilishaji matokeo hayo.

Akizungumza na waandishi habari, Mkurugenzi wa uchaguzi katika chama cha ODM Franklin Bett amesema matokeo yalianza kutangazwa huku shughuli ya kupiga kura ikiwa bado inaendelea jambo ambalo halijawahi kufanyika mahali popote ulimwenguni.

Mmoja wa wagombea wa urais Uhuru Kenyatta
Mmoja wa wagombea wa urais Uhuru KenyattaPicha: Getty Images

Bett amesema huo ni ukiukaji wa kanuni za uchaguzi na kwamba kufanya hivyo ni sawa na kuwashawishi wapigaji ambao hawakuwa wamepiga kura kufanya uamuzi tofauti.

Pia chama cha ODM kimelelamika kwamba kukwama kwa mitambo ya electroniki ya kutambua wapiga kura ni jambo jingine la kutiliwa shaka.

“Shughuli hiyo ilikumbwa na kasoro kuanzia awali wakati wa kupiga kura kuanzia asubuhi ambapo mitambo ya kuwatambua wapiga kura ilikwama na maafisa wa tume ya uchaguzi kulazimika kutumia daftari au sajili za wapiga kura badala ya mitambo ya electroniki. Sajili hiyo inaweza kuaminika vipi? Na huo ndio wasiwasi wetu.” Alisema Franklin Bett

Raila Odinga na mkewe baada ya kupiga kura jana
Raila Odinga na mkewe baada ya kupiga kura janaPicha: Reuters

Mkurugenzi huyo wa uchaguzi katika chama cha ODM, amesema kumekuwa na visa vya watu kupiga kura zaidi ya mara moja katika vituo kadhaa ambapo tume ya uchaguzi yenyewe awali ilikiri hayo na kwamba hilo pia ni jambo la kutiliwa shaka juu ya uhalali wa matokeo ambayo yamewasilishwa kufikia sasa.

Kwa upande wake tume ya IEBC hata hiyo imesisitiza kwamba matokeo yanayowasilishwa ni ya muda na hayawezi kuchukuliwa kuwa matokeo ya mwisho hadi maafisa wa uchaguzi watakapowasilisha stakabadhi zilizotiwa sahihi na waakilishi wa wagombea walioshiriki kwenye uchaguzi.

Kamishna wa IEBC Issack Hassan na Naibu wake James Oswago
Kamishna wa IEBC Issack Hassan na Naibu wake James OswagoPicha: James Shimanyula

Kwenye taarifa yake ya mwisho, Mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka Isaack Hassan alisema haya ni matokeo au takwimu za muda na wakenya wanapaswa kusubiri matokeo rasmi kutangazwa na tume ya uchaguzi punde tu maafisa wote wanaosimamia uchaguzi watakapowasilisha matokeo yao rasmi na hapo ndipo tume yake itakapotangaza mshindi na endapo hakutakuwa na mshindi tume itatangaza duru ya pili ya uchaguzi.

Matokeo yote ya uchaguzi nchini Kenya yanapokelewa hapa katika ukumbi wa Bomas moja kwa moja kutoka vituo vya kusehesabia kura katika majimbo mbali mbali kote nchini.

Mwandishi Alfred Kiti

Mhariri Amina Abubakar