1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kura zinahesabiwa nchini Zambia

Kalyango Siraj31 Oktoba 2008

Kiongozi wa upinzani aongoza

https://p.dw.com/p/FlCF
Hayati Levy Mwanawasa.Uchaguzi mkuu umefanywa ili kumchagua atakaechukua nafasi yakePicha: AP

Matokeo ya uchaguzi wa jana wa rais nchini Zambia yanaendelea kutolewa.Taarifa mpya kutoka huko zaonyesha kama kiongozi wa upinzani Michael Sata anaendelea kuongoza mpinzani wake, kaimu rais Rupia Banda.Uchaguzi huo unafuatia kifo cha hayati Levy Mwanawasa kilichosababishwa na ugonjwa wa kiharusi.

Matokeo ya awali yaliyotolewa leo Ijumaa yameonyesha kama kiongozi wa chama cha upinzani nchini humo Michael Sata anazidi kuongoza.

Matokeo kutoka theluthi mbili ya majimbo yote ya uchaguzi yanaonyesha kama kiongozi wa chama cha Patriotic Front akiwa mbele na kura 361,263. Huku kiongozi wa sasa wa chama tawala cha Movement for Multiparty Democracy MMD Rupiah banda akiwa na kura 240,941.Matokeo haya ni kutoka majimbo ya uchaguzi 43 kati ya majimbo yote 150.

Mengi ya majimbo yaliyokuwa yamehesabiwa yalikuwa katika ngome za sata katika mji mkuu wa Lusaka,pamoja na eneo la machimbo ya shaba.

Bwana Sata mwenye umri wa miaka 71 amejaribu mara mbili kutaka kuchaguliwa lakini mara hizo zote amekuwa akishindwa.Mara ya mwisho ulikuwa katika uchaguzi wa mwaka 2006 ambapo alibwagwa na marehemu Levy Mwanawasa ambae alifariki Agosti mwaka huu kutokana na ugonjwa wa kiharusi.Katika uchaguzi huo wa 2006 wafuasi wa Sata waliandamana wakipinga matokeo hayo.

Mara hii vikosi vya usalama viko chonjo dhidi ya ghasia zozote zinazoweza kutokea. Na Ingawa Sata anaongoza tayari amelalamika akidai kuwa kuna mizengwe inayopangwa ili kumnyima ushindi jambo ambalo amesema hatalikubali mara hii. Ameinyooshea kidole polisi pamoja na maafisa wa chama cha kitaifa kinachosimamia uchaguzi nchini humo.

Hata hivyo tume ya uchaguzi imekanusha madai hayo na msemaji wake Cris Akufuna amesema kuwa uchaguzi umeendelea bila matatizo.

Wachunguzi kutoka Umoja wa Afrika pia wanasema kuwa uchaguzi ulikuwa sawa bila matatizo na kutabiri kuwa 65% ya watu wote waliosajiliwa kupiga kura 3.9 millioni walipiga kura zao.

Nguvu za Sata zinatokana na kuwa anawawakilisha walala hoi.Ameahidi kuyalazimisha makampuni ya kigeni kutoa 25% ya hisa zao kwa wawekezaji wa ndani mwa Zambia.Pia ni mfuasi wa siasa za rais Robert Mugabe wa nchi jirani wa Zimbabwe.

Kwa upande wake mpinzani wake rais Banda nae mwenye umri wa miaka 71,alijipgia debe akisema kuwa atafuata nyayo za mtangulizi wake katika sera za uchumi. Sera za hayati Mwana wasa zimeisaidia nchi hiyo kupata maendeleo ya kutosha.Wiki chache kabla ya uchaguzi mkuu rais Banda alipunguza bei ya mbolea kwa 75%.