1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lahm: ninapanga kustaafu mwaka wa 2018

16 Januari 2015

Baada ya kustaafu kutoka soka la kimataifa aliposhinda Kombe la Dunia nchini Brazil, Philipp Lahm ametangaza kuwa anapanga kuzitundika njumu zake kabisa mwaka wa 2018, na kuiambia kwaheri klabu yake ya Bayern

https://p.dw.com/p/1ELlr
Phillip Lahm bricht Training ab
Picha: picture-alliance/dpa/D. Ebener

Lahm, akizungumza na gazeti la michezo la Ufaransa, L'equipe, amesema wakati huo atakuwa na umri wa miaka 34, na anahisi huo ndio wakati mzuri wa kustaafu kabisa kutoka kandanda.

Septemba 2014, Lahm aliliambia gazeti la michezo la Ujerumani “Sport Bild” kuwa alikuwa na uhakika angeweza kucheza kwa miaka mingine minne katika kiwango cha juu, na katika Bayern Munich kwa sababu ni klabu yake.

Licha ya kuwepo na mtindo wa wachezaji wenye umri mkubwa kuhamia Qatar au Marekani, Lahm anasema anataka kustaafu akiwa kileleni kama tu alivyofanya katika rangi za timu ya taifa ya Ujerumani.

Huku akiwa amesalia na miaka mitatu kwenye mkataba wake, nahodha huyo wa timu ya Ujerumani iliyonyanua Kombe la Dunia 2014 angali na ndoto kubwa katika klabu ya Bayern, ambayo ni kunyakua Kombe jingine la Ligi ya Mabingwa Ulaya – UEFA Champions League baada ya lile walilotwaa mwaka wa 2013.

Japokuwa Laham hatakuwa uwanjani kucheza akiwa na umri wa miaka 34, beki huyo amesema ni “bayana” kuwa atasalia katika mchezo huo kwa sababu “kandanda ni kitu anachokipenda”.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu