Lebanon kumchagua waziri mkuu mpya
31 Agosti 2020Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ziara yake hii nchini Lebanon ni ya pili katika kipindi cha chini ya mwezi mmoja. Aliwahi kuitembelea nchi hiyo katika ziara yake ya kihistoria iliyofanyika baada ya kutokea mripuko mkubwa kabisa uliouwa watu chungunzima katika bandari ya mjini Beirut, mripuko ambao ulisababisha kiwewe nchini Lebanon na kusababisha kuibua upya miito ya kufanyika mageuzi makubwa katika mfumo wa kisiasa nchini humo.
Majadiliano ya wabunge katika ikulu ya rais yanayohusu waziri mkuu mpya yalianza leo asubuhi huku vigogo wengi wa juu wa kundi la wachache wanaoitawala nchi hiyo wakionesha uwezekano wa tayari kukubaliana juu ya mwanadiplomasia asiyefahamika sana ambaye ni balozi wa Lebanon nchini Ujerumani Mustapha Adib.
Tayari bwana Adib anayesubiri kuidhinishwa leo baada ya mashauriano, hatakiwi na upinzani akiitwa ni zao la siasa zenye msingi wa kimadhehebu na kwa maana hiyo mwanadiplomasia huyo anakabiliwa na kazi ngumu ya kuiongoza nchi ikiwa katika mojawapo ya migogoro mikubwa kabisa ambayo haijapata kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 100 ya historia ya nchi hiyo.
Tukirudi nyuma kidogo ni kwamba mripuko wa bomu ulioutikisa mji wa Beirut uliotokea kwenye bandari ya mji huo,serikali inalaumiwa sana kwamba ulafi wake na kutowajibika kwake ndio chanzo cha tukio hilo pamoja na kuporomoka kwa uchumi wa taifa hilo katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita.
Kutokana na mgogoro uliopo Lebanon, rais wa Ufaransa Macron anayekwenda kwa mara nyingine nchini humo ametaka yafanyike mabadiliko makubwa na ya kina pale alipotoa tamko lake la tarehe 6 Agosti alipoitembelea nchi hiyo na kuonya kwamba atafuatilia hatua zilizopigwa pindi atakaporudi tena nchini humo kwa ajili ya kushiriki kumbukumbu ya miaka 100 tangu kuundwa kwa ile iliyojulikana kama dola kuu la Lebanon Septemba Mosi mwaka 1920.
Rais Michel Aoun na mshikira wake wa kisiasa kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah wote wamezungumzia nia na utayarifu wao wa kuunga mkono mabadiliko ya mfumo wa uongozi wa kisiasa nchini humo kupitia hotuba zao walizozitoa kila mmoja kivyake siku ya Jumapili.
Lakini pia kuna wanaotilia mashaka kauli zinazotolewa na vigogo wa juu nchini humo wanaohisi kwamba wanazungumzia kuunga mkono mageuzi kwa sababu tu ya ziara hii inayotarajiwa kufanywa na rais wa Ufaransa baadae siku ya Jumatatu.