1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leo ni siku 30 kabla ya kipyenga kupulizwa Afrika Kusini

11 Mei 2010

Leo umebakia mwezi mmoja kamili kabla ya kipyenga cha kuanza kwa fainali za kabumbu za kombe la dunia huko nchini Afrika Kusini.

https://p.dw.com/p/NL6P
Kombe la dunia la FIFAPicha: picture alliance/augenklick

Homa ya fainali hizo inazidi kupanda, huku ikiarifiwa kuwa jezi bandia zimetapakaa nchini Afrika Kusini kutakofanyika fainali hizo.

Bidhaa hizo bandia makhsusi kwa ajili ya fainali hizo zimetapakaa katika mitaa mbalimbali nchini humo, pamoja na kufanyika kwa msako kukabiliana na hali hiyo.

Mohamed Khader kutoka kampuni inayohusika na masuala ya sheria ya Spoor and Fisher inayoiwakilisha FIFA, amesema kuwa nyingi ya bidhaa hizo bandia zinatoka Asia.

Kwa mujibu wa wanasheria wa shirika hilo la kabumbu duniani, zaidi ya kesi 100 zinazohusiana na bidhaa bandia zimekwisha wasilishwa mahakamani tokea Januari mwaka huu.

Deutschland Joachim Loew Nationaltrainer Fussball EM
Joachim Loew kocha wa UjerumaniPicha: AP

Ukiachilia hayo, katika mawindo ya timu, Joachim Loew kocha wa Ujerumani, katika kikosi chake amechukua washambuliaji sita atakaokwenda nao katika fainali hizo.

Loew amesema ameamua kuwachukua washambuliaji hao sita ili awe na uwanja mpana zaidi wa kuweza kuwatumia washambuliaji hao kadri hali itakavyohitajika.

Amewaingiza katika kikosi chake Miroslav Klose na Lucas Podoski ambao msimu huu hawakuwika vilivyo. Wengine ni pamoja na Mario Gomez, Cacau, Stefan Kiessling na Thomas Muller.

Joachim Loew katika kikosi chake hicho ambacho ni miongoni mwa timu zinazopigiwa upatu kuondoka na mwari huko Afrika Kusini, amewateua wachezaji saba kutoka Bayern Munich, mabingwa wapya wa Bundesliga. Na hii anasema ni kutokana na kabumbu maridhawa lililooneshwa na wachezaji hao.

Loew amesema kuwa kwa kuwa na Lucas Podolski, Thomas na Cacau, timu ya Ujerumani itakuwa na washambuliaji watatu ambao wataweza pia kucheza pembeni, yaani wingi za kulia na kushoto. Miroslav Klose, Mario Gomez na Kiessling wao huwa ni washambuliaji wa kati na Joachim Loew anasema kuwa anataka kuwa na wachezaji imara pale itakapobidi kuwabadilisha.

Kiessling amewika msimu huu akiwa na Bayer Leverkusen, baada ya kupachika mabao 21, na kukamata nafasi ya pili ya wale waliyoufamania mlango mara nyingi zaidi katika msimu huu.

Ama huko nchini Uingereza, kocha wa timu ya taifa ya nchi hiyo, mtaliano Fabio Capelo, anajianda kutangaza kikosi chake hii leo na kusema kuwa fainali za kombe la dunia leo ndiyo zimeanza pamoja na kwamba kipyenga kitapulizwa rasmi siku 30 zijazo.

Capelo anakabiliwa na majeruhi kwa baadhi ya wachezaji muhimu kama vile Wayne Rooney, na kiungo wa Manchester City, Gareth Barry.Timu zitakazoshiriki fainali hizo zinatakiwa kuwasilisha majina ya vikosi vyao ifikapo mwisho wa mwezi huu, siku 11 kabla ya kipyenga kupulizwa na bila shaka na washabiki wa Afrika Kusini pia kuanza kurindima na vuvuzela zao.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/Reuters/ZPR

Mhariri:Othman, Miraji