1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Liberia kuanza kesi za uhalifu wa kivita miaka 5 ijayo

21 Desemba 2024

Mwanasheria aliyepewa jukumu la kuanzisha mahakama ya uhalifu wa kivita nchini Liberia amesema kesi za kwanza zitaanza kusikilizwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

https://p.dw.com/p/4oSvl
Rais Joseph Boakai wa Liberia
Rais Joseph Boakai wa Liberia.Picha: Olamikan Gbemiga/AP Photo/picture alliance

Jallah Barbu ambaye aliteuliwa mwezi Novomba na Rais Joseph Boakai kuanzisha mahakama hiyo ameyasema hayo alipozungumza na shirika la habari la AFP. Amesema ana matumaini kesi za kwanza zitasikilizwa kabla ya muhula wa sasa wa miaka sita wa rais Boakai haujamalizika.

Licha ya miaka kadhaa ya shinikizo la ndani na kimataifa, Liberia imeshindwa kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria wale waliofanya uhalifu wa kivita ikiwemo mauaji na ubakaji wakati wa mizozo iliyoligubika taifa hilo kati ya mwaka 1989 na 2003.

Inakadiriwa zaidi ya watu 250,000 waliuawa kwenye mizozo hiyo lakini imesadifu kuwa vigumu kuwatia hatiani wale waliohusika na kuwapatia haki wale waliopoteza wapendwa wao au kuathiriwa na vita.