1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ligi ya mabingwa "Champions League" kuanza Jumanne

12 Septemba 2011

Wolfsburg ya Felix Magath yashinda dhidi ya Schalke 04, mabingwa watetezi Borussia Dortmund yajikwaa nyumbani na Leverkusen yafanya mauaji dhidi ya Augsburg. Ligi ya mabingwa kuanza Jumanne

https://p.dw.com/p/12XXJ
Kocha wa VfL Wolfsburg alkifuatilia mchezo wa ligi.Picha: picture-alliance/dpa

Wolfsburg ya Felix Magath yashinda dhidi ya Schalke 04 katika Bundesliga, mabingwa watetezi Borussia Dortmund wajikwaa nyumbani na Leverkusen watoa kipigo kwa Augsburg.

Manchester United yazidi kuwatisha wapinzani katika premier League ,

Champions league kuanza rasmi kesho Jumanne , mabingwa watetezi Barca kuanza na AC Milan, Borussia Dortmund watakipiga na Arsenal London.

Meneja wa zamani wa Schalke 04 Magath amepata ushindi dhidi ya timu yake hiyo ya zamani , na huko Munich, walenga shabaha wa Bayern Munich waipa kisago Freiburg, Dortmund yapata kigugumizi na makamu bingwa Bayer Leverkusen wapata ushindi wa uhakika. Hayo ndio yaliyojiri katika mchezo watano wa ligi ya Ujerumani Bundesliga.

Licha ya Schalke kuongoza kwa bao 1-0 hadi kipindi cha kwanza kumalizika, walishindwa kuendeleza ubabe huo na kujikuta wanalala kwa mabao 2-1 dhidi ya timu ya sasa ya kocha wao wa zamani Felix Magath, Wolfsburg. Ilikuwa ni furaha tele kama anavyoeleza mlinzi wa Wolfsburg , Patrick Ochs.

"Tulishindwa katika michezo yetu mitatu iliyopita, tulikuwa na points tatu tu, na tulitaka kupanda juu. Na iwapo tungeshindwa leo ama kutoka sare, tungerudi nyuma sana. Lakini ulikuwa ushindi muhimu sana kwetu. Kila mtu ameona jinsi tulivyofurahia. Ulikuwa ushindi muhimu sana".

FC Kolon hata hivyo bado inasubiri ushindi wake wa kwanza nyumbani . Kwa kipigo cha mabao 2-1 nyumbani dhidi ya FC Nürnberg , FC Koln ilionyesha udhaifu mkubwa katika ulinzi na ingebugia mabao mengi zaidi iwapo isingezinduka katika dakika za mwisho.

FC Bayern ilikuwa na karamu ya magoli nyumbani , ilipokumbana na Freiburg , ambapo waliizawadia Freiburg mabao 7-0 mjini Munich, Mario Gomez akipachika mabao 4.

Mabingwa watetezi Borussia Dortmund walishangazwa na vijana waliopanda daraja msimu huu Hertha BSC Berlin kwa kupigwa mweleka wa mabao 2-1 nyumbani. Kocha wa Dortmund Jürgen Klopp amesema.

"Wakati haikuwa siku nzuri kwetu , ilikuwa siku nzuri sana kwa Hertha. Katika kipindi cha pili tulipata nafasi kadha nzuri, lakini hata Hertha nayo. Na ndio sababu ushindi wa leo ulikuwa halali kabisa kwa Hertha. Hili lazima tulikubali. Tutaendelea kufanya juhudi na kusonga mbele".

Werder Bremen iko katika nafasi sawa na Bayern Munich kwa points ikishika nafasi ya pili hata hivyo kutokana na wingi wa magoli ilionayo Bayern. Borussia Mönchengladbach inashika nafasi ya tatu baada ya kuipiga mwereka FC Kaiserslautern kwa bao 1-0. Hannover ilicharazwa mabao 3-0 na VFB Stuttgart. Mainz ilikiona cha mtema kuni kwa kukandikwa mabao 4-0 na Hoffenheim.

Meneja wa Manchester United Sir Alex Ferguson anaamini kuwa hali anayojikuta nayo Wayne Rooney hivi sasa katika soka la Uingereza ni muhimu kwa mshambuliaji huyo kuanza vizuri katika msumi huu. Rooney amekuwa mchezaji wa nne katika historia ya premier League kufunga mabao matatu katika kila mchezo wakati alipofunga mabao matatu katika ushindi siku ya Jumamosi dhidi ya Bolton Wanderers. Mshambuliaji huyo sasa amefikisha mabao manane katika michezo minne.

FC Zürich vs. FC Bayern München
Mshambuliaji hatari wa Bayern Munich Mario Gomez kulia, akipongezana na mchezaji mwenzake Müller.Picha: dapd

Nayo Manchester City iliinyoa bila maji Wigan Athletics kwa mabao 3-0. Chelsea ilijisogeza hadi nafasi ya pili baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Sunderland.

Nchini Hispania Real Sociedad ilipigana kiume baada ya kuwa nyuma kwa mabao 2-0 dhidi ya Barcelona na kufanikiwa kutoka sare na mabingwa hao kwa kufungana mabao 2-2. Real Madrid walijihakikishia kuendelea kubaki nafasi ya kwanza katika msimamo wa ligi kwa ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya mahasimu wao wa jadi Getafe. Betis Seville na Valencia zinashika kwa pamoja nafasi ya kwanza pamoja na Real Madrid zote zikiwa na points sita kila mmoja.

Kesho Jumanne ligi ya mabingwa katika bara la Ulaya inarejea uwanjani katika vita ya makundi. Mabingwa Barcelona inaanza utetezi wao wa taji la Champions League wakiwa nyumbani dhidi ya moja ya vigogo vya soka barani Ulaya AC Milan.

Fußball Sport FC Barcelona gegen FC Porto
Wachezaji wa mabingwa watetezi wa Champions League , FC Barcelona David Villa (kushoto) na Cesc Fabregas (kulia).Picha: picture alliance/dpa

Kikosi cha Pep Guardiola tayari kimetia kapuni mataji mawili msimu huu kombe la Super Cup la Hispania na lile la Ulaya, na Barcelona ina lenga kulinyakua kwa mara ya nne taji la Champions League katika muda wa miaka saba, lakini walionekana kupatwa na kigugumizi katika ligi ya nyumbani La Liga siku ya Jumamosi.

Barca mara nyingi imepata shida baada ya michezo ya timu za taifa, wakiugua kile kinachoitwa virusi vya FIFA, na uamuzi wa Pep Guardiola wa kuwapumzisha Leo Messi , David Villa na Andres Iniesta uliwashangaza wengi siku ya Jumamosi.

AC Milan ilianza kwa kusua sua katika ligi ya Italia baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Lazio Rome siku ya Ijumaa.

Ziara ya mjini Barcelona itakuwa kipimo kikubwa kwa kikosi cha kocha Massimilliano Allegri baada ya kuondolewa na mapema msimu uliopita na Tottenham Hotspurs katika timu 16 bora.

Mabingwa wa zamani Borussia Dortmund watakuwa wenyeji wa Arsenal London katika mchezo wao wa kundi F kesho Jumanne , timu zote zikihitaji kujitoa katika jinamizi la kufanya vibaya mwanzoni mwa msimu huu wa ligi. Mabingwa hao wa Champions League wa mwaka 1997 , waliangukia pua katika ligi baada ya kupata kipigo chao cha kwanza nyumbani msimu huu dhidi ya Heartha BSC Berlin iliyorejea msimu huu katika ligi daraja la kwanza.

Kocha Juergen Klopp atapata ahueni kwa kumpata tena Mario Goetze baada ya chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 19 kukosa pambano la ligi kutokana na kutumikia adhabu ya kukosa michezo miwili. Klopp amesema, tunaweza kucheza vizuri zaidi na kwa ubunifu zaidi.

Andre Villas-Boas anazindua juhudi zake katika kuwania taji la ubingwa wa Ulaya Champions League, mahali ambapo watangulizi wake sita wameshindwa kumkabidhi mmiliki wa Chelsea Roman Abramovich ubingwa huo. Tangu bilionie huyo kutoka Urusi kuchukua udhibiti wa club hiyo ya mjini London mwaka 2003, Claudio Ranieri , Jose Mourinho, Avram Grant, Luiz Felipe Scolari, Guus Hiddink na Carlo Ancelotti wameondoka Stamford Bridge baada ya kushindwa kufikia lengo hilo takatifu. Juhudi za hivi sasa za Chelsea kulipata taji hilo ambapo Abramovich ametumia mamilioni ya pauni kujaribu kushinda , itaanzia dhidi ya makamu bingwa wa ligi ya Ujerumani Bundesliga , Bayer Leverkusen uwanjani Stamford Bridge kesho Jumanne.

Tennis.

Serena Williams ameingia matatani na anakabiliwa na ukiukaji wa maadili kwa kumshambulia kwa maneno mwamuzi wa mchezo huo wa tennis Eva Asderaki katika seti ya pili ya mchezo huo jana na anakabiliwa na adhabu zaidi , ikiwa ni pamoja na faini pamoja na kuzuiwa kucheza. Mwamuzi wa mashindano ya US Open mwaka huu Brian Earley ametoa taarifa akisema kuwa anachunguza tukio hilo katika ukanda na anataka kuzungumza na Asderaki kuangalia iwapo Serena Williams atozwe faini.

Serena Williams Tennis
Serena Williams wakati wa mchezo jana kati yake na Samantha Stosur wa Australia katika mashindano ya U.S. OpenPicha: dapd

Uamuzi utatolewa leo Jumatatu.

Sam Stosur kutoka Australia amefanikiwa kumshinda Serena Williams na kunyakua ubingwa wa US Open jana Jumapili. Sam Stosur alishinda kwa seti mbili , 6-2 na 6-3.

Williams yuko kwa hivi sasa katika muda ambao hatakiwi kufanya makosa kama hayo kutokana na maneno machafu aliyoyatoa wakati wa mashindano ya US Open mwaka 2009 kufuatia kushindwa katika fainali ambapo Kim Clijsters aliibuka bingwa.

Alipigwa faini ya dola 82,500, na kuonywa kuwa faini hiyo inaweza kuongezwa maradufu na anaweza kusimamishwa kucheza mashindano mengine ya grand slam, iwapo atafanya makosa kama hayo katika kipindi cha miaka miwili. Hatua hiyo ilikuwa inamalizika baada ya mashindano haya ya US Open.

Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre / afpe / ZR/

Mhariri: Abdul-Rahman,Mohammed