1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Liverpool mabingwa wapya wa Ulaya

2 Juni 2019

Timu ya Liverpool imeshinda kombe la Klabu Bingwa barani Ulaya, Champions League baada ya kuifunga Tottenham Hotspur mabao 2-0 katika fainali zilizofanyika jana mjini Madrid, Uhispania.

https://p.dw.com/p/3JcHl
UEFA Champions League Finale | Tottenham Hotspur v FC Liverpool
Picha: Reuters/C. Recine

Goli la kwanza la Liverpool lilifungwa na Mohamed Salah dakika ya pili baada ya mchezo kuanza kwa mkwaju wa penalti ambayo ilisababishwa na Moussa Sissoko ambaye aliushika mpira kwenye eneo la hatari wakati mechi hiyo ikichezwa kwenye uwanja wa Wanda Metropolitano.

Divock Origi aliifungia Liverpool bao la pili katika dakika ya 87, ambalo liliipa ushindi timu hiyo. Origi aliingia uwanjani katika dakika ya 58 akitokea benchi

Liverpool ambayo imeshinda kombe hilo kwa mara ya sita katika historia ya klabu hiyo, mwaka uliopita ilipoteza katika fainali za Champions League baada ya kufungwa mabao 3-1 na Real Madrid mjini Kiev, Ukraine kutokana na Salah kulazimika kutoka nje baada ya kupata majeraha.

Kocha wa Tottenham, Mauricio Pochettino aliamua kumuanzisha Harry Kane, ingawa mshambuliaji huyo aliyekuwa akiuguza majeraha hajacheza katika mechi yoyote kwa kipindi cha miezi miwili, hatua ambayo hata hivyo haikuzaa matunda.

UEFA Champions League Finale | Tottenham Hotspur v FC Liverpool
Kocha wa Tottenham Hotspur, Mauricio PochettinoPicha: Getty Images/M. Hangst

Pochettino amesema timu yake ambayo ilikuwa ikipambana kuchukua ubingwa huo kwa mara ya kwanza, ilicheza vizuri hasa katika kipindi cha pili na imeonesha juhudi, hivyo anajivunia sana.

Liverpool ilifanikiwa kuingia katika fainali za Champions League baada ya kuifunga Barcelona ya Uhispania magoli 4-0, huku Tottenham Hotspur ikipata ushindi wa mabao 3 dhidi ya Ajax ya Amsterdam. Liverpool na Tottenham zote zinashiriki  katika Ligi Kuu ya England, Premier.

Fainali ya mwaka huu ni ya pili kufanyika katika kuzishirikisha timu za England, baada ya fainali ya mwaka 2008 zilizofanyika Moscow, Urusi ambapo Manchester United waliibuka washindi dhidi ya Chelsea.

Nchi nyingine ambazo ziliwahi kuziingiza klabu zake zote mbili katika fainali za Champions League ni pamoja na Uhispania, Italia na Ujerumani.

Klopp aondoa mkosi wa kufungwa

Huo ni ushindi wa kwanza kwa Liverpool chini ya kocha wake Mjerumani, Jurgen Klopp tangu alipojiunga na timu hiyo miaka mitatu na nusu iliyopita.

Hatimaye ushindi huo wa Liverpool umelisafisha jina la Klopp baada ya kupoteza michezo kwenye fainali sita katika miaka ya nyuma, zikiwemo mbili za kombe la klabu bingwa barani Ulaya.

Akizungumza na kituo cha televisheni cha michezo cha BT, Klopp alisema ''nina furaha kwa ajili ya vijana wangu, kwa ajili ya familia yangu, kwa sababu wamekuwa wakiumia kila mwaka tunapokwenda kwenye fainali''.

UEFA Champions League Finale | Tottenham Hotspur v FC Liverpool
Kocha wa Liverpool, Jurgen KloppPicha: Reuters/C. Recine

''Umewahi kuona timu kama hii? Unapambana kufa na kupona bila ya kuwa na mafuta kwenye tanki,'' alifafanua Klopp baada ya mchezo kumalizika. Amesema usiku wa jana huenda ukawa mzuri zaidi katika historia ya maisha yake.

Klopp kocha wa zamani wa Borussia Dortmund ameendelea kuiimarisha klabu ya Liverpool katika kipindi ambacho anaiongoza na hilo limedhihirika katika ushindi wa jana. Mara ya mwisho Liverpool ililinyakua kombe hilo mwaka 2005.

Klopp mwenye umri wa miaka 51 amesema kwa kawaida angekaa mbele ya waandishi habari kueleza ni kwa nini wamepoteza mchezo, lakini safari hii atapenda kueleza zaidi kuhusu ushindi wao. Aidha, amekiri kuwa kuna wakati ambao alijiona kama anashindwa kabisa na kujihisi kama bahati imemkimbia yeye na timu zake.

Furaha za mashabiki

Maelfu ya mashabiki wa Liverpool walimiminika katika mitaa ya Madrid kushangilia ushindi huo dhidi ya Tottenham huku wakiwa wamevalia nguo za rangi nyekundu wakiimba nyimbo za ushindi. Craig Williams shabiki wa Liverpool anasema haamini kama wameshinda tena.

Craig, mwenye umri wa miaka 32 aliyesafiri hadi Madrid akitokea Liverpool, Uingereza kwa ajili ya kushuhudia mechi hiyo, anasema wamefuta masikitiko waliyokuwa nayo mwaka uliopita.

Baadhi ya mashabiki walikuwa wamebeba vitu mbalimbali vinavyoonesha alama ya namba 6 kuashiria ushindi wa mara sita wa Liverpool katika fainali za kombe la Klabu Bingwa barani Ulaya. Mohammed Elneanaey, mwenye umri wa miaka 28 amesafiri kutoka Misri hadi Madrid kwa ajili ya fainali hiyo.

UEFA Champions League Finale | Tottenham Hotspur v FC Liverpool
Mashabiki wa LiverpoolPicha: Reuters/C. Recine

Hata hivyo, Mohamed ambaye anafanana na mchezaji wa Liverpool, Mohamed Salah alizongwa na mashabiki nje ya uwanja wakitaka wapige naye picha. Mashabiki kadhaa wa Liverpool ambao wamesafiri hadi Madrid kutoka maeneo mbalimbali duniani, wamesema wataendelea kubaki mjini humo hadi siku ya Jumatatu kwa lengo la kuendeleza shamrashamra za ushindi.

Viongozi nchini Uhispania wanakadiria kuwa kiasi ya tiketi 32,000 zilizokatwa na mashabiki wa timu zote mbili za Liverpool na Tottenham walihudhuria fainali hiyo katika uwanja wa Wanda Metropolitano wenye uwezo wa kuchukua watu 68,000.

Mamia ya safari za ziada za ndege kwenda kwenye mji mkuu wa Uhispania, Madrid ziliongezwa, na chama cha wamiliki wa hoteli mjini humo kinakadiria kwamba jumla ya mashabiki 70,000 wa Uingereza wataendelea kuwepo Madrid mwishoni mwa juma hili.