Liverpool yasherehekea ubingwa mitaani mjini Liverpool
3 Juni 2019Akiwa katika moja kati ya mabasi hayo, shujaa wa fainali hiyo Divock Origi mwenye asili ya Kenya amesema ni fahari kuitwa "lejendari wa Liverpool", kwa jukumu lake lililosababisha taji hilo kutua mjini Liverpool. Divock alisema
"Ni vizuri kufahamu hilo. Ni heshima kubwa. tunafahamu Liverpool ina maana gani kwa dunia kama klabu, kama klabu ya mpira, kwa hiyo nafikiri tuna furaha kwamba watu wanatoa matamshi kama hayo."
Mashabiki wa Liverpool walifyatua fashifashi na kuimba siku nzima katika mji huo ambao ulikuwa na rangi nyekundu kila mahali. Wachezaji kama Mo Salah, kocha Juergen Klopp, mlinzi Virgil van Dijk na wengine walishiriki katika shehere hizo kubwa, wakilionesha kombe wakiwa juu ya basi. Liverpool iliishinda Tottenham Hotspur pia ya England kwa mabao 2-0 katika fainali ya Champions League mjini Madrid siku ya Jumamosi.
Wakati huo huo mchezaji nguli wa kandanda wa Ujerumani Franz Beckenbauer amesema leo kwamba anataka kumuona kocha wa Liverpool Juergen Klopp katika benchi la ufundi la Bayern. Wakati Ujerumani ikisherehekea mafanikio ya Klopp katika champions league siku ya Jumamosi, Beckenbauer ameliambia gazeti la Bild kwamba anataka sana kumuona kocha huyo wa zamani wa Borussia Dortmund akijiunga na mabingwa wa Bundesliga , Bayern Munich.
"Sitaka kitu kingine zaidi ya kumuona Klopp akija Bayern siku moja, itakuwa kitu kizuri sana," amesema Beckenbauer mwenye umri wa miaka 73, ambaye alishinda ubingwa mara tano wa Bundesliga na Bayern akiwa kama mchezaji na kocha. Ubingwa wa kwanza wa Klopp wa Champions League ulisababisha sherehe kubwa katika vyombo vya habari za michezo nchini Ujerumani.
Na pia juhudi za Bayern Munich za kupata saini ya mshambuliaji wa Manchester City Leroy Sane zinaonekana kugonga mwamba, rais wa klabu hiyo Uli Hoeness amenukuliwa akisema katika ripoti leo Jumatatu.
"Unalazimika kuwa kidogo na shaka. Kuna uwezekano kwamba haitawezekana. Ni kuhusu wenda wazimu wa malipo ya uhamisho," gazeti la michezo la Kicker lilimnukuu Hoeness. Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, Manchester City inafanya juhudi mpya kurefusha mkataba wa mchezaji huyo wa kimataifa wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 23.