M23 wasalimu amri nchini Kongo
5 Novemba 2013Kundi hilo la waasi limesema katika taarifa yake kuwa "limeamua kuanzia leo kumaliza uasi wake" na badala yake litatimiza malengo yake "kupitia njia za kisiasa pekee". Hatua hiyo inamaliza uasi ambao umedumu miezi 18 na kuliharibu eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa raslimali na maliasili, lililokuwa kitovu cha mojawapo ya migogoro mibaya zaidi barani Afrika katika kipindi cha miongo miwili iliyopita.
Awali, serikali mjini Kinshasa ilidai "ushindi kamili" dhidi ya M23 baada ya kuyakomboa maeneo mawili ya milima yaliyokuwa yametwaliwa na wapiganaji hao.
Lambert Mende, waziri wa mawasiliano na msemaji wa serikali, amesema "wapiganaji wa mwisho wa M23 wameondoka katika ngome zao", akiongeza kuwa sasa "waasi hao wamekimbilia Rwanda."
Naye Luteni Kanali Olivier Amuli, msemaji wa jeshi katika eneo la Kivu ya Kaskazini ambaye alikuwa katika eneo la mapigano amesema "tumemaliza kazi". Amuli ameongeza kuwa kabla ya kutoroka, waasi hao walichoma moto na kuziangamiza kabisa silaha zao, vifaa na magari waliyokuwa wamepora wakati wakiudhibiti mji wa Goma.
Jeshi la Congo lilisaidiwa na MONUSCO
Jeshi la Congo lilianzisha mapingano makubwa dhidi ya waasi mnamo tarehe 25 Oktoba, na kwa haraka sana likaweza kuzikomboa ngome zao hadi pale waasi mwishoni mwa wiki iliyopita walipoelekea hadi maeneo matatu ya juu ya milima takribani kilomita 80 kaskazini mwa mji mkuu wa eneo hilo, Goma, na karibu na mpaka wa Rwanda.
Waasi hao waliozidiwa nguvu walisalimu amri, lakini jeshi likaendelea na mashambulizi yao, na kutwaa mojawapo ya eneo moja la juu yam lima Jumatatu.
Jeshi Maalum la Umoja wa Mataifa nchini Kongo (MONUSCO), ambalo limekuwa likiwasaidia wanajeshi wa Kongo kwa kufanya uchunguzi wa angani, ujasusi na mipango, lilijiunga katika uwanja wa mapambano Jumatatu usiku baada ya kupata idhini ya kuziripua ngome zilizosalia za waasi. Chanzo cha habari kutoka Kikosi hicho cha MONUSCO kimesema "wataendelea kuvurumisha mabomu na kufyatua risasi hadi kila kitu kitakapodhibitiwa."
Safisha safisha yaendelea
Operesheni za safisha safisha bado zinaendelea, ili kuhakikisha kwamba hamna mpiganaji yeyote wa M23 aliye na silaha mkononi katika maeneo yote ya wilaya ya Rutshuru, walikokuwa wakiendesha harakati zao. Siku ya Jumapili, kiongozi wa M23, Bertrand Bisimwa, alitangaza kuweka chini silaha ili kutoa nafasi ya kuanzishwa tena mazungumzo. Lakini mapigano yalionekana tu kuongezeka, hata baada ya ombi hilo la kiongozi wa M23, licha ya taarifa iliyotolewa mapema Jumatatu na wajumbe kutoka Umoja wa Ulaya, Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa iliyosema kuwa "wana wasiwasi kuhusu machafuko yaliyoanzishwa upya" ambayo yalifuatia amri hiyo ya kusitisha mapingano.
Kwa miongo mingi, eneo la Kivu ya Kaskazini na Kusini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limekuwa kitovu cha mzozo kwa sababu linazingirwa na mipaka ya Rwanda, Uganda, Burundi na Tanzania, pamoja na madini yanayopatikana kwa wingi katika milima ya eneo hilo.
Mwandishi: Bruce Amani/John Kanyunyu/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef