1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maambukizi mapya ya Covid-19 yavunja rekodi Ulaya,Marekani

Saleh Mwanamilongo
30 Oktoba 2020

Tangu janga la virusi vya corona kuripotiwa nchini Marekani, nchi hiyo imeorodhesha zaidi ya watu 90,000 walioambukizwa virusi hivyo katika muda wa saa 24.

https://p.dw.com/p/3kf8E
Schweiz, Genf I Hauptsitz der Weltgesundheitsorganisation I WHO I Gebäude
Picha: Reuters/D. Balibouse

Kwa mara ya kwanza tangu janga la virusi vya corona kuripotiwa nchini Marekani, nchi hiyo imeorodhesha zaidi ya watu 90,000 walioambukizwa virusi hivyo katika muda wa siku moja. Huku Ulaya ikiwa na wasiwasi kutokana na wimbi la pili la ugonjwa wa Covid -19 kwenye msimu huu wa baridi. 

Ikisalia siku  nne kabla ya uchaguzi wa Marekani, takwimu za Chuo Kikuu cha Johns Hopkins ,zinaonyesha katika saa 24 zilizopita, watu waliothibitika kuambukizwa virusi vya corona nchini Marekani ni 91,295. Chuo kikuu cha John Hopkins kimesema jumla ya watu milioni 8.94 wamepata maambukizi ya corona nchini humo.

Ufaransa imechukua hatua kali mpya za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona. Kuanzia leo Ijumaa Ufaransa imeweka vizuwizi hadi Desemba mosi ,ili kupunguza kasi ya maambukizi. Waziri mkuu Jean Castex amesema serikali ya Ufaransa huenda ikaanza kupunguza vikwazo hivyo pale maambukizi ya virusi vya corona yatakapoanza kupungua na kufikia 5,000 kwa siku. Kwa sasa yanaorodheshwa maambukizi 40,000 kwa siku. Idadi ya vifo nchini humo toka kuanza kwa ugonjwa huo imepindukia watu 36.000.

''Na nimuhimu kuweko na hatua za mshikamano'' 

Belgien Brüssel | EU Gipfel | Ursula von der Leyen
Picha: Dursun Aydemir/AA/picture-alliance

Mkuu  wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, amesema raia wa umoja huo, wanastahili kupunguza safari na badala yake wasafiri kwa mambo muhimu tu .

''Ongezeko la maambukizi ya virusi linaweza kunyemeleza mfumo wetu wa afya ikiwa hatutachukuwa hatua za haraka. Na nimuhimu kuweko na hatua za mshikamano katika Umoja wa Ulaya. Ndio kwa maana mpango wetu ulikuwa wa maana sana.''

Nchini Ujerumani nako, Taasisi ya Robert Koch inayoshughulikia janga la Covid-19 imesajili maambukizi mapya 18,681, ikiwa ndio idadi kubwa zaidi kuwahi kusajiliwa kwa siku moja. Kulingana na taasisi hiyo, karibu watu 500,000 wameambukizwa virusi vya corona kote Ujerumani, na miongoni mwao 11,349 wamekwishaaga dunia.Hata hivyo Ujerumani imepongeza,leo Ijumaa, kukua kwa uchumi wake kwenye robo ya tatu ya mwaka.

Tunisia yaweka amri ya kutotoka nje usiku

Uispania imetangaza pia hatua kali za vizuwizi kwenye majimbo matano, ikiwemo Madrid. Bunge la nchi hiyo liliindinisha jana kurefushwa kwa hali ya dharura ya kiafya kwa kipindi cha miezi sita.

 Nchini Ubeljiji hatua mpya zinatarajiwa kuchukuliwa mwishoni mwa wiki hii,licha ya kwamba migahawa, maeneo ya maonyesho na michezo tayari yamefungwa.

Kuingineko,nchini Urusi visa vya maambukizi kwa siku vilifikia 18.000 leo Ijumaa, Iran iliorodhesha visa 8.300 kwa siku, huku Tunisia ikianzisha amri ya kutotoka nje usiku. Nchini Sri Lanka, mji mkuu Colombo umewekewa vizuwizi vya siku tatu.