1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mabenki yafunguliwa tena Cyprus

MjahidA28 Machi 2013

Benki nchini Cyprus zimefunguliwa tena chini ya ulinzi mkali huku wateja wakikabiliwa na masharti ya namna ya kudhibiti pesa zao. Wateja hao hawatakuwa na nafasi ya kuchukua kiwango kikubwa cha fedha kwa mara moja.

https://p.dw.com/p/185Rk
Benki nchini Cyprus
Benki nchini CyprusPicha: Yiannis Kourtoglou/AFP/GettyImages

Wafanyakazi katika benki nchini Cyprus waliwahimiza wateja kutokuwa na hamaki wakati watakapokuwa wakichukua kiwango kidogo cha fedha walichotengewa kutowa kila siku, baada ya kutokuwa na uwezo wa kufanya hivyo kwa siku 12 wakati benki hizo zilipokuwa zimefungwa.

Benki hizo zilifungwa kwa muda wa wiki mbili wakati serikali ikijadili mkopo wa uokozi wa euro bilioni 10, ambao ni wa kwanza katika kanda ya euro, kuwatia hasara wateja wa benki.

Watu wakipiga kambi nje ya mabenki, Cyprus
Watu wakipiga kambi nje ya mabenki, CyprusPicha: picture alliance/dpa

Hata hivyo masoko ya dunia yalikuwa na wasiwasi mkubwa baada ya kuona udhibiti wa dhamana uliowekwa kwa mara ya kwanza kwa uchumi wa ulaya ili kuzuia kuanguka kwa uchumi wa Cyprus baada ya kupata mkopo wa uokozi wa euro billioni 10, kutoka kwa Umoja wa Ulaya na shirika la fedha la Kimataifa IMF.

Masharti kwa wateja wa mabenki Cyprus

Sasa amri ya wizara ya fedha nchini humo imeweka kikomo cha uchukuaji fedha, kwa kila raia kuwa na nafasi ya kutoa euro 300 tu kwa siku, na hakuna malipo ya hundi au cheki yanayokubalika.

Benki Kuu ya Cyprus itaridhia malipo yote yanayozidi euro 5,000, na kuchunguza malipo ambayo yatakwenda juu ya euro 200,000 huku watu wanaoondoka nchini Cyprus wanaruhusiwa kuchukua kiwango cha euro 1,000 pekee. Masharti haya yatadumu muda wa wiki moja kabla ya kujadiliwa tena.

Rais wa Cyprus Nicos Anastasiades
Rais wa Cyprus Nicos AnastasiadesPicha: AFP/Getty Images

Hii leo asubuhi benki zote katika mji wa Nicosia zilikuwa na maaskari wawili au watatu wengi wao wakiwa na silaha nje ya milango ya benki hiyo. Taswira hiyo imetoa hali ya wasi wasi katika eneo ambalo limekuwa likishuhudia amani na ambalo ni kitovu cha watalii wengi.

Roula Spyrou, raia wa nchi hiyo aliye na umri wa miaka 50 anayemiliki duka moja la dhahabu amesema hatajishughulisha kamwe kwenda benki.

Bunge la Cyprus
Bunge la CyprusPicha: AFP/Freier Fotograf

"Siwezi kwenda benki hii leo, kutakuwa na watu wengi sana na siwezi kupanga laini hadi jioni kuchukua euro 300 tu," Alisema Roula Spyrou.

Kwa upande wake utawala nchini humo kupitia televisheni ya kitaifa hapo jana jioni ilitoa wito kwa raia wake kutoa nafasi kwa wazee katika kuchukua kiwango kidogo cha fedha walichotengewa kuchukua kila siku na serikali.

Kamisheni ya Ulaya yazungumzia Cyprus

Huku hayo yakiarifiwa Kamisheni ya Ulaya imesema itaangalia kwa karibu dhamana inayodhibitiwa na benki hiyo kama njia moja ya kuokoa kuporomkoka kwa uchumi wa Cyprus.

Katika taarifa yake kamisheni hiyo imesema kuwa itashirikiana na serikali ya Cyprus pamoja na mataifa mengine ya ulaya, benki kuu ya ulaya, pamoja na utawala wa mabenki ya ulaya kuangalia kwa karibu utekelezwaji wa mpango wa kukaza mkwaja kwa dhamana katika mabenki nchini humo ili kujaribu kuokoa uchumi wa nchi hiyo kuanguka.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef