Machafuko Gabon baada ya matokeo kutangazwa.
4 Septemba 2009Kumezuka machafuko mapya na uporaji katika mji wa Port Gentil ambao ni nguzo ya kiuchumi kwa Gabon huku wafuasi wa upinzani wakiendelea kupinga matokeo ya uchaguzi wa Jumapili uliopita , baada ya tume ya uchaguzi kumtangaza Ali Bongo, mtoto wa rais wa zamani Omar Bongo Odimba kuwa mshindi.
Machafuko hayo katika mji huo wa Port Gentil yametokea licha ya kutangazwa amri ya kutotoka nje,huku vituo vya mafuta vikichomwa moto na katika sehemu nyingi za mji huo yakiporwa. Mchana huu harakati za kawaida mji humo zilionekana kuwa ndogo mno na hakuna hata Taxi moja iliokua barabarani. Maduka yote yamefungwa. Kamanda wa polisi mjini humo Luteni Kanali Nguima Mambinga alisema watu 23 akiwemo mmoja mwenye asili ya Cameroun wametiwa nguvuni. Pia Polisi imewakamata vijana wengine kiasi ya 30 wenye umri kati ya miaka 14 na 30. Polisi na wanajeshi wanaendelea kupiga doria, wakati hali ikiwa bado ni ya wasi wasi.
Ufaransa mkoloni wa zamani wa Gabon, imetangaza kwamba inayakubali matokeo ya uchaguzi huo. Waziri wa mambo ya nchi za nje Bernard Kouchner alisema msimamo huo unatokana na taarifa ya ujumbe wa watazamaji katika uchaguzi huo ambao wameridhishwa na zoezi lilivyofanyika.
Bw Kouchner aliyesema kuwa ingawa kulikua na uchelewesha katika maandalizi na utekelezaji wea zoezi hilo lakini uchaguzi ulikua wa uwazi na akasisitiza kwamba Ufaransa haikua na mgombea katika uchaguzi huo, matamshi yanayoashiria kujibu madai kwamba ikimuunga mkono Ali Bongo, mtoto wa rais wa zamani Omar Bongo aliyetawala kwa muda wa miaka 41 na kufariki dunia mwezi Juni.
Ufaransa ina masilahi ya kisiasa na kiuchumi nchini Gabon ikiwa na kituo cha kijeshi na kampuni ya mafuta ya Ufaransa,Total ina kandarasi ya uchimbaji mafuta katika taifa hilo . Ufaransa imewaamuru raia wake wapatao 10,000 nchini Gabon kuondoka. Vijana wenye hasira jana waliuchoma moto ubalozi mdogo wa nchi hiyo na kutoa matamshi ya vitisho dhidi ya wazungu.
Waziri wa mambo ya nchi za nje Kouchner amesema Ufaransa kwa sasa haina mpango wa kuwahamisha raia wake walioko Gabon, lakini iko tayari kufanya hivyo wakati wowote itakapohitajika.
Akizunguzmza na Deutsche Welle kiongozi wa upinzani Pierre Mamboundou aliyegtokea watatu alisema Ali Bongo amekamilisha mpango wake na kuongeza, "Nafikiri Ali Bongo ameheshimu alichokipanga nacho ni mapinduzi ya kura.Sisi tutaendelea kulalamika na tunalalamika pia kupitia chombo chenu cha habari."
Mwansiasa kutoka nchi jirani ya Senegal Aisata Sal Tal, amelalamika juu ya kuzuka mtindo mpya ambao anasema ni kitisho kwa demokrasia. " Nafikiri ni mfano mbaya kwa Afrika na demokrasia. Naifikiria Senegal, Misri na hata Tunisia na kila nchi ambako kuna mipango ya Viongozi wa taifa kuwaweka madarakani watoto au marafiki zao. Nafikiria juu ya viongozi wote wa taifa ambao wanafikiri wanaweza kufanya watakalo na katiba za nchi zao."
Ali Bongo alitangazwa mshindi kwa asili mia 42, akifuatwa na waziri wa zamani wa mambo ya Andre Mba Obame asili mia 26 na Pierre Mamboundo nafasi ya tatu akiwa na asili mia 25 ya kura. Machafuko mjini Libreville na Port Gentil yalianza mara tu baada ya tume ya uchaguzi kutangaza matokeo.
Mwandishi:M.Abdul-Rahman /AFP
Mhariri :Othman Miraji