1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Machar aapishwa makamu wa rais Sudan Kusini

Admin.WagnerD26 Aprili 2016

Kiongozi wa waasi wa Sudan Kusini Riek Machar ameapishwa kuwa makamu wa kwanza wa rais Jumanne, baada ya kurejea Juba kwa mara ya kwanza, tangu kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe zaidi ya miaka miwili iliyopita.

https://p.dw.com/p/1Id0E
Oppositionsführer Riek Machar bei PK
Picha: imago/Xinhua

Machar ambaye amerudi katika nafasi aliyoishikilia kabla ya mgogoro huo, alipokelewa mjini Juba Jumanne mchana na mawaziri pamoja na wanadiplomasia na kuelekea moja kwa moja katika ikulu ya rais, ambako aliapishwa sambamba na hasimu wake mkuu rais Salva Kiir. Kurudi kwake kumecheleweshwa kwa wiki nzima, na kutishia makubaliano ya amani yaliyojadiliwa kwa muda mrefu.

Akizungumza baada ya kuapishwa, Machar aliahidi kuyatekeleza kikamilifu makubaliano ya amani, ili kuwezesha kuanza haraka kwa mchakato wa maridhiano na kutibu madonda ya vita hivyo. Kwa upande wake rais Kiir alisema kwa vile Machar amekula kiapo cha makamu wa rais, kinachofuata sasa ni kuunda haraka serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa.

Kamanda mkuu wa jeshi la Machar Simon Gatwech Dual akizungumzia ujio wa Machar hapo awali.
Kamanda mkuu wa jeshi la Machar Simon Gatwech Dual akizungumzia ujio wa Machar hapo awali.Picha: picture-alliance/dpa/P. Dhil

Usalama wa Machar

Machar alitanguliwa na kamanda wa juu wa waasi Simon Gatwech Dual, aliewasili mjini Juba siku Jumatatu. Waasi walisema alisindikizwa na wanajeshi karibu 200 ambao wamepangwa kutoa ulinzi kwa Machar.

Wanajeshi hao ambao walikuja na bunduki 20 za rasharasha na mitambo 20 ya kufyatua roketi, walitarajiwa kuungana na wanajeshi zaidi ya 1300 wa waasi, waliowasili mjini Juba mapema kama sehemu ya makubaliano ya amani.

Marekani na Umoja wa Mataifa ziliongeza shinikizo kwa Machar kurudi Juba bila kuchelewa, na Marekani ilikwenda mbali zaidi ikisema katika taarifa iliotolewa na wizara ya mambo ya nje kuwa kiwango cha ushiriki wa taifa hilo katika kuisadia Sudan Kusini kutatua changamoto zake za kiusalama, kiuchumi na maendeleo, utategemea dhamira ya pande mbili kushirkiana katika utekelezaji wa makubaliano ya amani.

Matumaini ya kumaliza vita

Mkuu wa kitengo cha ulinzi wa amani cha Umoja wa Mataifa Herve Ladsous, amesema kurejea kwa Machar mjini Juba laazima kusafishe njia kwa kipindi cha mpito wa kweli kukomesha vita nchini humo.

Rais Kiir (kulia) na Machar (kushoto) wakati wakiwa bado wanaelelwana.
Rais Kiir (kulia) na Machar (kushoto) wakati wakiwa bado wanaelelwana.Picha: picture-alliance/AP Photo/P. Muller

Kiir na Machar walisaini makubaliano ya amani mwezi Agosti, lakini hayakumaliza kabisaa mapigano na utekelezaji wake ulicheleweshwa. Maelfu ya watu wameuawa katika mgogoro huo uliyoanza Desemba 2013, wakati vikosi vya usalama vilipoonekana kugawanyika kwa misingi ya ukabila. Machar aliitoroka nchi na kuwa kiongozi wa uasi mkali sana.

Pande zote mbili zimetuhumiwa kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu, na kwa mujibu wa shirika la hisani la Oxfam, watu wasiopungua milioni 2.8 nchini kote wanapambana kupata chakula cha kutosha.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,adpe,dpae

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman