1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Machar arejea Sudan Kusini

John Juma RTRE/AFPE/DPAE
31 Oktoba 2018

Machar aliwasili katika uwanja wa ndege mapema leo akiongozana  na wanachama wa kundi lake la SPLM na alikaribishwa na maafisa wa serikali.

https://p.dw.com/p/37QH9
Südsudan Rückkehr von Riek Machar
Picha: Reuters/S. Bol

Kiongozi wa waasi wa Sudan Kusini Riek Machar, amewasili leo mjini Juba kushiriki shughuli za sherehe za kitaifa za amani. Hii ni mara ya kwanza Machar amerejea Juba baada ya miaka miwili tangu alipokimbia nchi yake.

Machar aliwasili katika uwanja wa ndege mapema leo akiongozana  na wanachama wa kundi lake la SPLM na alikaribishwa na maafisa wa serikali.

Maelfu ya watu walimiminika barabarani mjini Juba kwa shangwe, huku wakicheza na kuimba nyimbo za amani.

Usalama uliimarishwa maradufu katika mji huo, wanajeshi wenye silaha wakipiga  doria huku ndege za kijeshi zikipaa angani.

Machar na kundi lake sasa watahudhuria shughuli za sherehe ya amani pamoja na serikali ambapo wanatarajiwa kutoa hotuba.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilizuka baada ya rais Kiir kumlaumu Machar kutaka kumpindua
Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilizuka baada ya rais Kiir kumlaumu Machar kutaka kumpinduaPicha: Reuters/S. Bol

Kurudi kwa Machar katika nchi hiyo inayokumbwa na machafuko, kumejiri baada ya waasi na serikali kutiliana saini makubaliano ya amani mnamo mwezi Septemba, kumaliza mapigano ya wenyewe kwa wenyewe ambayo yamedumu kwa miaka mitano.

Sudan Kusini ambayo ndiyo nchi changa zaidi duniani ilitumbukia katika machafuko mwaka 2013 baada ya rais Salva Kiir kumlaumu aliyekuwa makamu wake Riek Machar, kuwa alipanga njama ya kumpindua. Machar aliikimbia Sudan Kusini na kuelekea nchi jirani ya Congo mnamo Julai 2016.

Machar atasalia Juba baada ya sherehe?

Viongozi wengine wa kanda hiyo wanatarajiwa kujiunga na Machar na rais Kiir kwenye sherehe ya kuunga mkono hadharani makubaliano ya amani.

Haijabainika wazi ikiwa Machar atasalia mjini Juba baada ya sherehe. Tayari maafisa wake wameelezea wasiwasi kuhusu usalama wake mjini humo.

Makubaliano kadhaa ya awali kati ya kundi la Machar na Kiir ya kusitisha mapigano yamevunjika
Makubaliano kadhaa ya awali kati ya kundi la Machar na Kiir ya kusitisha mapigano yamevunjikaPicha: picture-alliance/M. Hjaj

Awali, sherehe iliyopangwa ya kumkaribisha Machar nchini humo, iliahirishwa kufuatia mvutano kuhusu idadi ya askari wake wanaomlinda wanaoruhusiwa kumsindikiza  na idadi ya silaha wanazoruhusiwa kuzibeba.

Makubaliano yaliyosainiwa mwezi Septemba sasa yanaruhusu kuundwa kwa serikali ya mpito, ambapo Machar atarejea katika wadhifa wake wa zamani wa makamu wa rais.

Mashaka ya waangalizi wa kimataifa

Hata hivyo waangalizi wengi wa kimataifa wana mashaka ikiwa makubaliano hayo yatadumu ikizingatiwa chama cha Machar kilitilia mashaka baadhi ya vipengee vya makubaliano hayo.

Makubaliano ya awali yalivunjika baada ya pande zinazozozana kushindwa kuyaheshimu na mikataba mingi ya kusitisha mapigano ikavunjika.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Sudan Kusini vimesababisha vifo vya maelfu ya watu, na takriban watu milioni 4 wa nchi hiyo kukimbia mapigano.

Makundi ya kutetea haki za binadamu yameripoti visa vibaya vya ukiukaji wa haki za binadamu vinavyofanywa na pande zote mbili, serikali na waasi.

 

Mhariri: Yusuf Saumu