1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron asema yuko tayari kujadiliana na wote

12 Mei 2017

Rais mteule wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema yuko tayari kuzungumza na wanasiasa wanaoelemea siasa za kihafidhina nchini mwake ili kuwashawishi washiriki katika uchaguzi wa bunge wa mwezi ujao.

https://p.dw.com/p/2cqxP
Frankreich Emmanuel Macron hält Rede nach Wahl
Picha: REUTERS/Pool/L. Bonaventure

Huku mvutano ukiwa unatokotota baina pande hizo mbili za kisiasa nchini Ufaransa  rais mteule wa Ufaransa ambaye hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana alikuwa waziri wa uchumi katika serikali ya kisoshalisti alivunja utamaduni uliozoeleka kwa kushinda katika uchaguzi wa rais uliomalizika Jumapili iliyopita kwa kuendesha kampeni zake bila kuelemea kwenye chama chochote cha kisiasa. Macron alianzisha vuguvugu lake linalojulikana kama Republic On the Move (REM) kwa maana ya Taifa Linalosonga Mbele.

Msemaji wa Macron, Arnaud Leroy amesema lipo kundi la wanasiasa wa kihafidhina ambao hawaelemei siasa zenye mtazamo mkali na ambao wanataka kujumuika katika maendeleo ya Ufaransa lakini hawataki kujiunga na vuguvugu la Macron kwa hivyo rais mteule yuko tayari kujadiliana na wanasiasa wa aina hiyo.

Frankreich Politiker Richard Ferrand von Macrons Bewegung En Marche
Katibu mkuu wa vuguvugu la REM Richard FerrandPicha: Getty Images/AFP/E. Feferberg

Lengo kuu la Macron sio kuwatenga wanasiasa wa kihafidhina bali anataka vuguvugu lake liwe na viti vingi baada ya uchaguzi wa bunge unaotarajiwa kufanyika mwezi Juni ili aweze kufanikisha kuzipitisha hoja kadhaa zinazolenga kuleta mageuzi katika sekta ya uchumi kwa mujibu wa katibu mkuu wa vuguvugu lake, Richard Ferrand.  Ferrand amesema lengo lao ni kukijengea nguvu chama cha REM bungeni ili waweze kuwa na sauti katika bunge hilo la taifa.  Hapo jana, majina 428 ya wanasiasa wanaotaka kugombea chini ya mwamvuli wa vuguvugu la REM yalipendekezwa. Wengi kati ya wagombea hao hawajulikani kabisa katika medani za kisiasa. Kuna jumla ya majimbo 577 nchini Ufaransa yatakayogombewa. Kati ya majina hayo yaliyopendekezwa, 24 ni wanasiasa walioondoka kutoka kwenye chama cha Kisoshalisti kinachoongozwa na rais anayemaliza muda wake, Francois Hollande.

Huku zikiwa zimesalia siku mbili tu kabla ya Macron kuapishwa, mpaka sasa jina la waziri mkuu na mawaziri ambao wataunda serikali yake ya kwanza bado yamewekwa siri. Hata baadhi ya maswahiba wa rais huyo mteule na watu ambao anawaamini bado hawajaambiwa kile kinachotarajiwa. Katibu mkuu wa vuguvugu la REM Richard Ferrand amesema hata yeye hajui ni nani atakayepewa wadhifa wa uwaziri mkuu na amesema anafikiri hivyo ni vizuri.

Mwandishi: Zainab Aziz/APE/RTRE
Mhariri: Mohammed Khelef