Macron asisitiza uwepo Djibouti Ufaransa ikitimuliwa Afrika
21 Desemba 2024Macron alifanya ziara kifupi katika taifa hilo la Pembe ya Afrika kwa mazungumzo na Rais Ismail Omar Guelleh na kukutana na wanajeshi wa Ufaransa kabla ya sikukuu za mwisho wa mwaka.
Hivi karibuni, mataifa kadhaa ya Afrika yamevunja makubaliano ya kijeshi na Ufaransa na kuamuru wanajeshi wake waondoke.
Macron alisema wakati wa mazungumzo na Guelleh kuwa uwepo wa Ufaransa nchini Djiboutini muhimu kwa usalama wa njia za biashara za Indo-Pasifiki kati ya Ulaya na Asia.
"Uwepo huu Djibouti bila shaka pia unalenga Bahari ya Hindi, Indo-Pasifiki," alisema Macron.
Aliongeza kuwa mkakati wa Ufaransa katika Indo-Pasifiki "hauwezi kufanikiwa bila vikosi vya Ufaransa nchini Djibouti".
Soma pia: Macron amsifu Abiy kwa mageuzi ya kihistoria Ethiopia
Macron aliwaambia wanajeshi wa Ufaransa siku ya Ijumaa kwamba kituo hicho kinaweza kupata umuhimu mkubwa zaidi kwa kuwa kinaweza "kubuniwa upya" kuwa kituo cha uzinduzi wa operesheni barani Afrika.
"Katika nchi kadhaa, tulikuwa na vituo vya kihistoria vilivyojengwa. Tumetaka kufikiria upya ruwaza hiyo," alisema.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa Djibouti si sehemu ya mipango hiyo "kwani kwa miongo kadhaa muundo wa kituo chetu hapa na operesheni zetu ni tofauti kabisa".
Djibouti inaangalia ukanda mkubwa wa Bahari ya Hindi — eneo linalojumuisha India, China, na njia za baharini zinazochangia sehemu kubwa ya biashara ya dunia.
Wanajeshi wa Ufaransa waliondoka Mali, Burkina Faso, na Niger mnamo 2022 na 2023 baada ya serikali za kijeshi zilizochukua madaraka katika nchi hizo kuvunja makubaliano ya ulinzi na mkoloni huyo wa zamani.
Nchini Chad, imeanza kuondoa ndege za kivita na wanajeshi katika wiki za hivi karibuni baada ya kiongozi wa kijeshi wa nchi hiyo kukata mahusiano ya kijeshi. Senegal pia ilitoa ombi kama hilo mnamo Novemba.
Soma pia: China yafungua kituo cha kwanza cha kijeshi Djibouti
Rais wa Djibouti alisisitiza "uhusiano wa kipekee" wa nchi yake ndogo na Ufaransa. Makubaliano ya ulinzi yalirefushwa mnamo Julai.
Mkataba wa ujenzi wa uwanja mpya wa ndege na maendeleo ya shirika la anga ulisainiwa Jumamosi.
Viongozi hao wawili pia walijadili matatizo ya kikanda, ikiwa ni pamoja na vita nchini Sudan.