1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron azuru Lebanon

6 Agosti 2020

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amewasili mjini Beirut, siku chache baada ya mlipuko uliosababisha vifo vya kiasi ya watu 137 na kutoa mwito wa kuchukuliwa hatua za haraka za kurejesha utulivu na uthabiti nchini humo.

https://p.dw.com/p/3gVpd
Frankreich Präsident Emmanuel Macron
Picha: picture-alliance/abaca/F. Crusiaux

Lebanon hii leo inawaomboleza wahanga wa mlipuko mbaya kabisa nchini humo ambayo tayari inakabiliwa na mzozo mbaya wa kiuchumi katika wakati ambapo vikosi vya uokozi vikiendelea kuwatafuta watu wasiojulikana walipo tangu mripuko huo ulipotokea na kuiharibu vibaya bandari na jiji la Beirut.

Waziri mkuu Hassan Diab alitangaza siku tatu za maombolezo kuanzia hii leo kwa ajili ya wahanga wa mlipuko huo ambao ni mbaya kabisa kuwahi kushuhudiwa kwenye jiji la Beirut ambalo bado linakabiliwa na vitisho kadha wa kadha ikiwa ni pamoja na kuporomoka kwa uchumi na kuongezeka kwa visa vya maambukizi ya virusi vya corona.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron tayari amewasili mjini Beirut kwa ziara ya kikazi na kuwa kiongozi wa kwanza wa kigeni kufanya ziara nchini humo tangu mlipuko huo wa Jumanne uliosababisha vifo vya kiasi ya watu 137 na watu 5,000 kujeruhiwa.

Libanon Beirut Ausmaß der Zerstörungen nach Explosion im Hafenviertel
Eneo la bandari lililoharibiwa vibaya na mripuko, mjini Beirut na kusababisha vifo vya takriban watu 137Picha: Reuters/A. Taher

Amesema, taifa hilo linakabiliwa na mzozo wa kiuchumi na iwapo hakutafanyika mageuzi, Lebanon itaendelea kukabiliwa na machafuko na kuongeza kuwa hatua za haraka zinatakiwa kuchukuliwa. Alikuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasili Beirut.

Urusi jana usiku ilituma ndege yenye hospitali zinazohamishika pamoja na watoa huduma za afya. Kulingana na wizara ya masuala ya dharura ya Urusi mapema jana, taifa hilo lilikuwa linatuma ndege tano za misaada kuelekea Lebanon. Ndege nyingine iliyokuwa na vifaa vya kupima virusi vya corona iliondoka mji wa Saratov, Urusi mapema leo.

Libanon Beirut nach der Explosion im Hafenviertel
Vikosi vya uokozi vimeendelea kuwatafuta wahanga wa mripuko huo waliofukiwa chini ya vifusiPicha: Reuters/A. Tahir

Naibu mkuu wa kituo cha kitaifa cha udhibiti cha Urusi Sergei Vorontsov, amesema watumishi wote wa afya wanaokwenda Lebanon watapewa vifaa vya kujilinda na maambukizi ya virusi hivyo, alisema "Sergei: Tuna taarifa kwamba kuna watu bado wamefukiwa na vifusi. Kwa hiyo tunaenda kule na kwanza tutatumia kikosi chetu cha mbwa na ndege zisizo na rubani lakini pia tutasimama kimya kwa dakika chache, wakati tunapokwenda kuwatafuta manusura wa janga hili."

Bado mamia hawajulikani walipo na hadi robo ya watu wapatao milioni moja wameachwa bila ya makazi yanayofaa kuishi baada ya kishindo cha mlipuko huo kuharibu majengo na madirisha yaliyokuwa umbali wa hadi maili moja katika eneo la bara nchini humo. Maafisa wanasema, huenda idadi ya vifo ikaongezeka.

Aidha, Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la afya, WHO umepeleka tani 20 za vifaa vya tiba kwa ajili ya watu waliojeruhiwa kwenye mripuko huo ambavyo ni pamoja na vya upasuaji.

Maafisa wameitupia lawama serikali kwa janga hilo, kufuatia mrundikano wa kemikali hatari za mlipuko zilizohifadhiwa kwa miaka kadhaa kwenye eneo la bandari katika mazingira yasiyo salama. vyanzo kutoka wizarani vililiambia shirika la habari la Reuters kuwa serikali iliagiza maafisa wa bandarini kuwekwa kifungo cha nyumbani.

Hata hivyo, raia aliyejulikana kwa jina moja Azar alisema hawatarajii chochote hata baada ya uchunguzi bali mtu mmoja tu atatolewa kama kafara ili serikali ijitenge na uwajibikaji.

Mashirika: RTRE/DPAE.