Maelfu ya waandamanaji Korea Kusini wakusanyika Seoul
4 Januari 2025Maelfu ya waandamanaji, wanaomuunga mkono na wale wanaompinga Yoon, walikusanyika mbele ya makazi yake na kwenye barabara kuu za mjini Seoul, wakizingirwa na mamia ya maafisa wa usalama watiifu kwa rais huyona ambao mpaka sasa wamezuia juhudi za waendesha mashitaka kumkamata.
Wanachama wa jumuiya ya vyama vya wafanyakazi nchini Korea, walijaribu kutembea kuelekea makazi ya Yoon kuandamana dhidi yake, lakini walizuiwa na polisi. Wapelelezi kutoka Ofisi ya Kuchunguza vitendo vya rushwa, wamemuomba waziri wa fedha Choi Sang-mok, ambaye anashikilia wadhifa wa kaimu rais tangu wiki moja iliyopita, kuunga mkono waranti wa kumkamata Yoon.
Mpaka sasa, kitengo cha ulinzi wa rais huyo kimekataa kutoa ushirikiano. Kitengo hicho kimesema maafisa wake wawili wakuu walikataa ombi la kufika mbele ya polisi leo ili kuhojiwa, wakitaja changamoto kubwa ya kumlinda rais huyo anayekabiliwa na mashitaka ya uasi na jinai.