Mafuriko yaathiri maelfu ya watu nchini Jamhuri ya Kongo
13 Januari 2024Umoja wa Mataifa umesema kuwa mafuriko yaliyoenea katika nchi ya Jamhuri ya Kongo yamesababisha maelfu ya raia kuhitaji msaada wa haraka. Mvua kubwa zisizo za kawaida zimesababisha idara tisa kati ya 12 za nchi hiyo kuathirika.
Mafuriko hayo yameharibu miundombinu 34 ya hospitali, shule 120 na nyumba zaidi ya elfu 64. Watu zaidi ya laki tatu wameathirika moja kwa moja na kadhia hiyo. Mvua hiyo kubwa ni mara mbili ya kiwango cha wastani kilichorekodiwa kati ya mwaka 2022 na 2023.
Soma: Mamia wapoteza maisha kufuatia mafuriko Kongo
Mafuriko hayo yalitokea kwenye kingo za mito ya Kongo karibu na Mto Ubangi huku Umoja wa Mataifa ukionya kuwa inaweza kusababisha kuzuka kwa magonjwa ya milipuko kama vile kipindupindu na kuzorotesha upatikanaji wa huduma za afya. Watu 17 wamefariki tangu mafuriko yalipotokea.