1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mafuriko yasababisha maafa magharibi mwa Kenya

Musa Naviye11 Aprili 2023

Takribani familia 180 zinazoishi kwenye fukwe za Ziwa Viktoria jimbo la Siaya eneo la Nyanza huko Kenya zimeachwa bila makaazi baada ya mvua nyingi inayonyesha maeneo mbali mbali nchini humo kusababisha mafuriko.

https://p.dw.com/p/4Pu93
Archivbild, Überschwemmungen in Afrika
Picha: AP

Mvua nyingi ambayo imekuwa ikinyesha kuanzia mwezi Machi hadi Aprili mwaka huu eneo la Magharibi mwa Kenya imesababisha kufurika kwa Ziwa Viktoria na kuwalazimisha wakaazi wa vijiji vya Got Agulu wadi ya Yimbo jimboni Siaya kutafuta makaazi mengine maeneo salama huku makundi ya uokoaji kutoka shirika la Msalaba Mwekundu na mamlaka ya usimamizi wa majanga yakihamishia waathiriwa kwenye soko la Ulowa.

Kulingana na wakaazi wa hapa, mafuriko hayo yamechangia hatari ya maradhi kama vile Malaria kutokana na ongezeko la mbu pamoja na kukabiliwa na hatari ya kuvamiwa na mamba, viboko na nyoka ambao wanafuata mafuriko hayo hadi vijijini huku shughuli zao za kutafuta kipato kutokana na uvuvi Ziwani Viktoria zikiathirika kipindi hichi ambapo taifa linakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi.

Soma pia: Waathiriwa wa mafuriko Marsabit wapewa chakula cha msaada

Präsidentschaftswahl in Kenia
James Orengo akiwa na Kithure KindikiPicha: John Ochieng/SOPA Images via ZUMA Press Wire/picture alliance

Serikali ya jimbo la Siaya ikiongozwa na Gavana James Orengo imeanzisha mpango wa kutoa misaada ya chakula, vyandarua, na mablanketi kwa wakaazi walioathirka huku akisema kuna haja ya ushirkiano na serikali ya kitaifa kufikia suluhisho la kudumu kwa mafuriko ya mara kwa mara eneo hilo.

Kadhalika, ameitaka serikali ya kitaifa kukamilisha ujenzi wa kivuuko kinachounganisha Ziwa Sare na Ziwa Viktoria kufanya hivyo ameeleza kutasaidia kukabiliana na mafuriko hayo, wakati ukarabati wa mikondo ya kuelekeza maji hayo ukiendelea.

Athari ya mafuriko inashuhudiwa huku idara ya hali ya hewa ikionya kuwa, mvua nyingi zaidi itaendelea kushuhudiwa na hivyo mafuriko zaidi yanatarajiwa eneo la Magharibi mwa Kenya mvua hiyo ikiandamana na ngurumo za radi.