1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magaidi waua tena mjini Paris

Abdu Said Mtullya7 Januari 2015

Watu 12 wameuawa kutokana na shambulio la kigaidi lililofanyika kwenye ofisi za jarida moja mjini Paris. Kwa mujibu wa taarifa, watu wengine zaidi ya 10 walijeruhiwa katika shambulio hilo.

https://p.dw.com/p/1EGEo
Polisi wakiwasaidi wahamga wa shambulizi la kigaidi
Polisi wakiwasaidi wahamga wa shambulizi la kigaidiPicha: Reuters/J. Naegelen

Katika shambulio hilo polisi wawili pia waliuawa. Wachoraji vibonzo wanne wa gazeti hilo, ikiwa pamoja na mhariri mkuu ni miongoni mwa watu walioauwa.

Rais Francois wa Ufaransa amesema mauaji hayo ni kitendo cha kigaidi. Polisi ya mjini Paris imeliambia shirika la habari la AFP kuwa mauaji hayo yalitokea kwenye ofisi za jarida la tashtiti linalotolewa kila wiki mjini Paris .

Habari zaidi zinasema jarida hilo, "Charlie Hebdo" liliwahi kushambuliwa kwa bomu mnamo mwaka wa 2011 baada ya kuchapisha vibonzo vya kumtashtiti Mtume wa dini ya kiislamu .

Rais Hollande atembelea ofisi za jarida la Charlie Hebdo
Rais Hollande atembelea ofisi za jarida la Charlie HebdoPicha: K. Tribouillard/AFP/Getty Images

Rais Hollande alieenda haraka kwenye ofisi za gazeti la "Charlie Hebdo" amesema waliofanya mashambulio hayo ya kigaidi watasakwa mpaka watakamatwa na kufikishwa mahakamani.

Washambuliaji walikuwa na silaha nzito

Kwa mujibu wa taarifa ya polisi washambuliaji walikuwa zaidi ya watu wawili, waliokuwa na bunduki aina ya Kalashnikov na zana za kurushia roketi.

Watu hao waliokuwa wamezifunika nyuso zao walizivamia ofisi za gazeti la "Charlie Hebdo" na kuanza kushambulia. Muda mfupi baadae mapambano yalitokea baina ya magaidi hao na polisi.

Kwa mujibu wa taarifa ya polisi watu hao walisikika wakisema kuwa walifanya shambulio hilo ili kulipiza kisasi kwa niaba ya Mtume wa dini ya kiislamu. Mohammad. Baada ya kufanya mauaji, magaidi hao walitoweka. Waliingia katika gari na kukimbia na mpaka sasa bado hawajakamatwa.

Majeruhi aondolewa baada ya shambulio
Majeruhi aondolewa baada ya shambulioPicha: picture-alliance/dpa/AP Photo/T. Camus

Ufaransa imeimarisha ulinzi kwenye nyumba za ibada, kwenye maduka na kwenye vituo vya usafiri katika mji wa Paris. Rais Hollande alieliezea shambulio la leo kuwa ni la kikatili anakutana na baraza lake la mawaziri ili kuijadili kadhia iliyotukia.

Viongozi wa dunia walaani shambulio

Viongozi kadhaa ikiwa pamoja na Rais Vladimir Putin wa Urusi wamelaani vikali shambulio hilo la kigaidi. Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron akizungumza bungeni amesema Uingereza ipo pamoja na watu wa Ufaransa.

Cameron amesema Uingereza imesimama pamoja na watu wa Ufaransa katika kupinga aina zote za ugaidi na imesimama kidete katika kuunga mkono uhuru wa kutoa maoni na demokrasia

Polisi watembelea eneo lililoshambuliwa mjini Paris
Polisi watembelea eneo lililoshambuliwa mjini ParisPicha: Reuters/C. Hartmann

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amelaani shambulio la mjini Paris kuwa ni hujuma dhidi ya uhuru wa kutoa maoni.

Kansela Merkel amesema katika ujumbe kwamba shambulio hilo ni hujuma siyo tu dhidi ya wananchi wa Ufaransa bali pia dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari.

Mwandishi:Mtullya abdu./afp,rtre,ZA

Mhariri: Gakuba Daniel