Mahakama Ulaya: Shambulizi la Kunduz lilikuwa sahihi
16 Februari 2021Uamuzi uliotolewa Jumanne na mahakama hiyo ya haki za binadamu ya Ulaya mjini Strassburg umekuja baada ya miaka kadhaa ya mapambano ya kisheria katika mahakama za Ujerumani ambazo zilitoa uamuzi kwamba Kanali wa kikosi chake Georg Klein aliyehusika katika mashambulizi hayo hakufanya kosa.
Leo hii mahakama hiyo ya mjini Strassburg imeonesha kuiunga mkono Ujerumani ambapo katika uamuzi wake imesema mahakama za Ujerumani na waendesha mashtaka wake walifanya uchunguzi wa kina kuhusu mashambulizi hayo ya Septemba 4 mwaka 2009 yaliyofanywa na jeshi la kikosi cha wanaanga cha Marekani nchini Afghanistan ambayo yaliwauwa raia kadhaa.
Kesi hii iliyotolewa uamuzi wake leo ilifunguliwa katika mahakama hiyo ya haki za binadamu ya Ulaya na bwana mmoja wa Kiafghanistan kwa jina Abdul Hanan,ambaye watoto wake wawili waliuwawa katika tukio hilo la shambulizi la kijeshi.
Bwana huyo alifungua kesi kwa hoja kwamba Ujerumani iliwapokonya wanawe hao wawili wakiume waliokuwa na umri wa miaka 8 na 12, haki ya kuishi pamoja na kumyima yeye haki ya kudai fidia.
Hata hivyo mahakama hiyo ya haki za binadamu baada ya kuisikiliza kesi hii imesema Ujerumani haikufanya ukiukaji wowote wa kifungu nambari 2 cha mkataba unaosimamia haki za binadamu barani Ulaya na zaidi ya hayo mamlaka za Ujerumani zilizingatia yote yaliyohitajika katika kufanya uchunguzi wa kiuhakika chini ya sheria za mkataba huo.
Uamuzi huu sasa ndio wa mwisho kuhusu kesi hiyo na hauwezi kukatiwa rufaa. Wolfgang Kaleck,mkuu wa kituo cha kutetea katiba na haki za binadamu barani Ulaya ambaye pia muda wote akimpa msaada wa kisheria Hanan amesema uamuzi wa mahakama ya Strassburg ni wa kukatisha tamaa kwa mlalamika na wanakijiji wenzie,ingawa amegusia kwamba majaji wameweka wazi serikali zinawajibu wa alau kuchunguza matukio kama haya.
Katika mkasa huo wa Kunduz,kamanda wa kijerumani,kanali Klein aliamrisha ndege za kivita za Marekani kuyashambulia malori mawili yaliobeba mafuta yalioonekana huko Kunduz baada ya kutekwa nyara huko Kusini mwa Afghanistan,tukio ambalo lilisababisha mripuko mkubwa.
Ripoti za awali zilieleza kwamba wengi waliouwawa katika tukio hilo walikuwa wapiganaji wa Taliban lakini baadae zikaibuka taarifa kwamba wahanga wengi walikuwa ni raia wa kawaida waliokuwa wamekusanyika wakiwa na matumaini ya kuchota mafuta ya kwenda kutumia majumbani.
Ujerumani ilianzisha mchakato wa kumchunguza Klein nchini Ujerumani huku familia za wahanga zikikimbilia kwenye mahakama za Ujerumani kudai fidia lakini mara zote kesi zao zikishindwa na kesi ya karibuni kabisa nchini Ujerumani iliamualiwa Desemba.
Wakati huo mahakama ya Ujerumani ilipitisha uamuzi kwamba haikumkuta na hatia ya uzembe Kamanda Klein na wala sheria ya Ujerumani hairuhusu kesi za watu binafsi dhidi ya nchi ya kigeni. Kadhalika toka wakati huo, Kanali Klein alipandishwa cheo na kuwa brigedia jenerali.