Mahakama ya Cameroon imezikataa rufaa 18 ya uchaguzi
19 Oktoba 2018Mahakama ya katiba nchini Cameroon imezikataa rufaa 18 ya mwisho kutaka kurudiwa kwa sehemu au uchaguzi mzima wa urais uliofanyika Oktoba 7, ambao wapinzani wanadai uligubikwa na udanganyifu.
Hatua hiyo sasa inafungua njia kwa maafisa kutangaza matokeo ya uchaguzi kabla ya Jumapili, ambayo kwa kiasi kikubwa yanatarajiwa kuongeza muda kwa rais ambaye tayari ametawala taifa hilo kwa miaka 37, Paul Biya.
Awali, mwanasheria wa kiongozi wa upinzani alisema mahakamani kuwa wanaharakati wanaotaka kujitenga wanaozungumza lugha ya Kiingereza wameichoma moto nyumba ya kiongozi wa zamani wa upinzani na kumchukua mateka dada yake mnamo siku ya Jumatano.
Kiongozi huyo John Fru Ndi, aliyeongoza chama cha Social Democratic Front, SDF, anayetokea eneo la magharibi linalokaliwa na wanaozungumza Kiingereza, ingawa amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya rais Paul Biya, wanaharakati hao wanamuona kama msaliti kwa kuwa anakubaliana na kurejeshwa kwa suluhu ya mfumo wa serikali ya shirikisho nchini humo, wakati wao wanapigania kuundwa kwa taifa huru la wanaotumia lugha ya Kiingereza.