1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama ya kijeshi Kivu yamshitaki afisa wa FARDC

7 Julai 2021

Afisa huyo anashitakiwa kwa makosa ya uzembe yaliosababisha kupotea kwa silaha na vifaa mbalimbali vya kijeshi vya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

https://p.dw.com/p/3w9Pe
DRK Symbolbild FARDC
Picha: Alain Wandimoyi/AFP

Mahakama ya kijeshi katika mkoa wa Kivu Kusini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo imemshtaki afisa wa jeshi la serikali FARDC, Luteni kanali Musumbuko Muhindo Edmond, kwa uzembe uliosababisha kupotea kwa silaha na vifaa mbalimbali, wakati akiwa kamanda wa kikosi cha FARDC katika wilaya ya Fizi mwaka 2020.

Kapteni Dieudonné Kasereka, ameiambia DW kwamba afisa huyo anashtakiwa kwa sababu baadhi ya vifaa vya kikosi chake, zikiwemo silaha, risasi, na sare za kijeshi, vilipelekwa mahali pasipo julikana na wengi wa askari wa kikosi chake wakajiunga na afisa mwingine, Michel Rukundo Makanika aliyeasi jeshi la Kongo wakati huo na kwenda msituni.

Mahakama ya kijeshi katika mkoa huo inategemea kuwa kesi hii itatoa mwangaza kamili kuhusu idadi ya vifaa vya kijeshi vilivyokwishauzwa kwa wanamgambo msituni na kwamba itakuwa fundisho kwa sababu kuna askari wengine na hata pia raia ambao bado wanatajwa mara kwa mara katika shughuli za ununuzi na uuzaji wa zana za kijeshi, hasa katika wilaya za Fizi, Uvira na Mwenga.

Chanzo: Mitima Delachance/DW