Mahakama ya kijeshi Misri yawahukumu kifo watu 17
11 Oktoba 2018Mahakama ya kijeshi ya Misri imewahukumu kifo watu 17 leo kuhusiana na mashambulio kadhaa ya mabomu ya kujitoa muhanga katika makanisa.
Kundi la Dola la Kiislamu lilidai kuhusika na mashambulizi hayo ambayo yalisababisha watu kadhaa kufariki.
Watu wengine 19 wamehukumiwa kifungo cha maisha na wengine 10 wamehukumiwa kifungo cha miaka kuanzia 10 hadi 15.
Watu 74 waliuwawa katika mashambulizi mwaka 2016 na 2017 mjini Cairo, Alexandria na mji ulioko ukingoni mwa mto Nile wa Tanta. Waliolengwa ni Wakristo wa madhehebu ya Coptic, ambao ni asilimia 10 ya wakaazi wa Misri ambao wakaazi wake wengi ni Waislamu wa madhehebu ya Sunni.
Tangu kuondolewa madarakani kwa kiongozi mfuasi wa nadharia za Kiislamu Mohammed Mursi mwaka 2013, mamia ya polisi , wanajeshi na raia wameuwawa katika mashambulizi ya wapiganaji wa jihadi.