1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama yamtaka Zuma ajibu mashtaka

Admin.WagnerD29 Aprili 2016

Mahakama , Afrika Kusini imeamua Rais Zuma atapaswa kujibu mashtaka yaliyotupiliwa mbali mnamo mwaka wa 2009. Hata hivyo chama chake cha ANC kimesema uamuzi huo hauna maana kuwa Zuma ana makosa.

https://p.dw.com/p/1IfS9
Picha: picture-alliance/dpa/N. Bothma

Mashtaka juu ya kashfa iliyohusu mkataba wa silaha wa mabilioni ya fedha yalifutiliwa mbali na mwendesha mashtaka mkuu wa serikali, hatua iliyomfungulia njia bwana Zuma ya kuchaguliwa kuwa Rais, wiki chache tu baadae.

Akitoa hukumu, Hakimu wa Mahakama Kuu Aubrey Ledwaba alisema uamuzi wa kusimamisha kesi dhidi ya Zuma ulikuwa kinyume cha mantiki. Hakimu huyo amesema Rais Zuma lazima afikishwe mahakamani kujibu mashtaka.

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani, Democratic Alliance, Mmusi Maimane amesema lazima Zuma afikiswhe mahakamani. Maimane ameeleza kuwa mtu yeyote, au Rais yeyote hapaswi kuwa juu ya sheria. Amesema wanachi wote wanapaswa kuwa sawa mbele ya sheria na kwa hivyo uamuzi wa kusimamisha kesi dhidi ya Zuma ulienda kinyume na mantiki.

Uamuzi uliotangazwa na Hakimu Aubrey Ledwaba unawaruhusu waendesha mashtaka kuanzisha tena kesi ya ufisadi dhidi ya Rais Jacob Zuma. Kesi hiyo ilifikishwa mahakamani na chama cha upinzani cha Democratic Alliance,DA.

Zuma azidi kuzama katika dimbwi la matata.

Rais Zuma tayari amebanwa kutokana na uamuzi wa Mahakama ya katiba kwamba Rais huyo alikiuka katiba, kwa sababu ya kushindwa kulipa fedha za umma alizotumia kwa ajili ya kukikarabati kijiji chake binafsi katika jimbo la lake za uzawa la Kwa -Zulu.

Kiongozi wa chama cha upinzani cha Democratic Alliance Mmusi Maimane
Kiongozi wa chama cha upinzani cha Democratic Alliance Mmusi MaimanePicha: Getty Images/AFP/M. Safodien

Mwendesha mashtaka aliuhalalisha uamuzi wa kuisimamisha kesi iliyokuwa inamkabili Zuma kwa sababu simu zilizodakizwa kati ya maafisa waandamizi wa utawala wa Rais Thabo Mbeki, zilionyesha ujiingizaji wa kisiasa katika kesi hiyo.

Nakala za simu hizo zilizoitwa "kanda za ujasusi",zilifichwa,lakini hatimaye zilitolewa hadharani mnamo mwaka wa 2014 na kukabidhiwa kwa chama kikuu cha upinzani, DA baada ya miaka mitano ya mapambano ya kisheria.

Kiongozi wa chama hicho Maimane amesema uamuzi uliotolewa na mahakama ni pigo kubwa kwa Rais Zuma.

Shinikizo la kumtaka Rais Zuma ajiuzulu linazidi kuongezeka na mashujaa kadhaa wa chama kilichomwezesha Madiba kuingia madarakani mnamo mwaka 1994 wanaunga mkono. Zuma anaepaswa kuimaliza mihula yake miwili mnamo mwaka wa 2019, hataweza kugombea tena urais.

Hata hivyo chama chake cha ANC kilichojaa makada wanaomtii, kinaweza kumwondoa madarakani kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu. Chama hicho kimesema baada ya kutangazwa hukumu dhidi ya Zuma kuwa haitaathiri nafasi yake katika uchaguzi ujao wa serikali za mitaa.

Mwandishi:Mtullya Abdu./afpe/ rtre.

Mhariri:Idd Ssessanga