Mahakama yaridhia Kabila kuendelea madarakani
18 Oktoba 2016Vyama vinavyounda muungano tawala katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na vyama vingine vidogo vimekubaliana kuchelewesha uchaguzi wa mwezi ujao hadi Aprili mwaka 2018. Vyama hivyo vimetia saini makubaliano hayo mjini Kinshasa leo(18.10.2016). Makubaliano hayo yanatoa nafasi kwa Rais Joseph Kabila kusalia madarakani hadi uchaguzi mpya utakapofanyika.
Mkataba huo ulipitishwa baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa takriban siku 40, chini ya usimamizi wa mjumbe wa Umoja wa Afrika Edem Kodjo, licha ya kususiwa na vyama muhimu vya upinzani, kikiwemo UDPS cha kinara wa upinzani Etienne Tshisekedi. Makubaliano hayo hayafafanui iwapo rais Kabila anaweza kuwania muhula mwingine baada ya mwaka huo.
Mahakama ya katiba katika nchi hiyo vile vile imekubali ombi lililowasilishwa na tume ya taifa ya uchaguzi la kuahirishwa uchaguzi wa rais na bunge uliotarajiwa kufanyika mwaka huu. Hata hivyo mahakama hiyo imeitaka tume hiyo ya uchaguzi kutangaza kalenda mpya ya uchaguzi.
Vyama ambavyo havikushiriki katika majadiliano hayo vinadai kwamba Rais Kabila kubaki madarakani kupindukia muda wake anaoruhusiwa na katiba ni kukiuka katiba ya nchi hiyo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / DW Kinshasa correspondent.
Mhariri: Daniel Gakuba.