Maisha katika wakati wa COVID-19
Tangu mwishoni mwa 2019 vilipozuka virusi vya corona, watu zaidi ya million 100 wameshaambukizwa - na kuyageuza maisha juu chini, chini juu.
Kuweka umbali kutoka mtu mmoja hadi mwengine
Singapore imerikodi viwango vya chini kabisa vya maambukizi ya virusi vya corona tangu Oktoba. Wangaalizi wameisifu nchi hiyo kwa kudhibiti virusi hivyo. Mafanikio hayo yanatokana na jitihada ya kuwafuatilia kwa karibu raia kupitia App maalumu. Kupungua kwa maambukizi kunamaanisha raia wanaweza kwenda kwenye sinema zilizo wazi – huku wakiweka umbali kutoka mtu mmoja hadi mwengine.
Wasiwasi umetanda Afrika Kusini
Afrika Kusini ni taifa la Afrika lilopigwa vibaya zaidi na janga la virusi vya corona. Mgonjwa huyu aliye hospitali ya karibu na Cape Town ni mmoja wa wagonjwa milioni 1.4 waliopata ugonjwa wa COVID-19. Na kuzuka kwa aina mpya ya kirusi kiitwacho B.1.351 au 501Y.V2, kumeongeza wasiwasi mno nchini humo. Kwani aina hiyo mpya inatajwa kuwa na kasi zaidi ya maambukizi.
'Kuweka umbali kati ya watu kwenye jua kali'
Joto la kiangazi likiwa linaongezeka, wengi nchini Australia wameanza kwenda kuogelea baharini. Lakini pia kumewekwa vibango vya tahadhari kuwakumbusha waogeleaji waweke umbali kutoka mtu mmoja hadi mwingine wakiwa ufukweni, ili kuzuia idadi ya maambukizi. Idadi ya maambukizi mapya imepungua nchini humo tangu Septemba.
Uchungu wa kuondokewa na mzazi
Kelvia Andrea Goncalves, 16, analia karibu na kaburi la mama yake nchini Brazil katika mji wa Manus. Andrea dos Reis Brasao alifariki akiwa na umri wa miaka 39. Hospitali mjini humo zimeelemewa na kukosa oksijeni ya kuwasaidia wagonjwa kupumua. Wengi wanamlaumu Rais Jair Bolsonaro kwa kuruhusu hali kuwa mbaya sana. Zaidi ya watu 221,000 wamefariki Brazil kutokana na virusi vya corona.
Je, kinga ni bora kuliko tiba?
Huko Hong Kong, mamlaka zimefungia mitaa kadhaa kutotoka nje bila ya onyo, baada ya ghafla maambukizi kuongezeka. Hong Kong imechukuwa hatua kali na sawa na zile ilizochukuwa China kudhibiti virusi hivyo. Na hadi hivi karibuni, viwango vya maambukizi vilikuwa vya chini sana.
Kucheza mziki kwenye povu
Bendi ya miondoko ya rock nchini Marekani The Flaming Lips imevumbua njia ya kufanya show huku ikihakikisha mashabiki wake wanaweka umbali kutoka mtu mmoja hadi mwingine. Kila shabiki ametakiwa kusimama kwenye plastiki lenye umbo mithili ya povu. Kwa namna hiyo kila mmoja anakuwa amejitenga mbali na mwenziwe.
Makanisa yaligeuza vituo vya chanjo
Kwa vile makanisa mengi yamefungwa kutokana na janga la virusi vya corona, maeneo ya ibada yamegeuzwa kuwa vituo vya chanjo ya dharura. Kwa mfano hapa kwenye Kanisa Kuu la Lichfield, karibu na Birmingham, Uingereza. Tofauti na nchi za Umoja wa Ulaya ambazo zinakabiliwa na uhaba wa chanjo za COVID-19, Uingereza imepokea chanjo za kutosha.
Kuna mwanga mwishoni mwa handaki ya giza
Amy Ezzat anatengeneza keki mfano wa chanjo ya virusi vya corona ambayo watapelekewa wagonjwa wa COVID-19 wanaopatiwa matibabu katika hospitali mjini Cairo. Misri inakabiliwa na changamoto nyingi ikijaribu kuanzisha kampeni ya nchi nzima ya kutoa chanjo. Lakini wengi nchini humo bado hawakukata tamaa ya kupata chanjo hiyo.