1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Malaga yaiteka Dortmund

4 Aprili 2013

Borussia Dortmund wamebaki wakijikuna vichwa kutokana na nafasi walizokosa kutumia katika mchuwano wa mkondo wa kwanza wa robo fainali ya Champions League dhidi ya Malaga, ambapo walitoka sare ya bila kufungana

https://p.dw.com/p/189Dq
[38565333] Spain Soccer Champions League Malaga's Jeremy Toulalan, center, is challenged by Dortmund's Felipe Santana of Brazil, right, during the Champions League quarterfinal first leg soccer match between Malaga CF and Borussia Dortmund in Malaga, Spain, Wednesday, April 3, 2013. (AP Photo/Miguel Angel Morenatti)
Fußball Champions League Malaga CF gegen Borussia DortmundPicha: picture alliance/AP Photo

Matokeo hayo yana maana kuwa mchuwano bado uko wazi wakati timu hizo zitakapokutana nyumbani kwa Dortmund Jumanne wiki ijayo kwa mkondo wa pili, ijapokuwa Dortmund huenda wakajuta ni kwa nini hawakufunga goli la ugenini.

Borussia hata hivyo imebaki kuwa timu pekee katika Champions League msimu huu ambayo haijashindwa mchuwano wowote, wakati Malaga ikiendeleza rekodi yake ya kutoshindwa mchuwano wa nyumbani barani Ulaya kufikia mechi 14.Mkufunzi wa Malaga Manuel Pellegrini anasema mchuwano wa mkondo wa pili nchini Ujerumani hautakuwa tofauti na ule wa jana nchini Uhispania. Anasema timu zote zilikuwa na nafasi nzuri za kufunga mabao.

Timu zote mbili zilikosa nafasi za wazi kufunga mabao
Timu zote mbili zilikosa nafasi za wazi kufunga mabaoPicha: picture-alliance/dpa

Safu ya mashambulizi ya Dortmund ikiongozwa na Mario Götze na Robert Lewandowski ilisababisha usumbufu mkubwa katika lango la Malaga na kumfanyisha kazi ya ziada kipa Willy Caballero. Akizungumza baada ya mechi, Götze ambaye alitupa nafasi mbili za kutikisa wavu katika kipindi cha kwanza akiwa yeye na kipa pekee, amesema angeisaidia sana timu yake kwa kufunga goli la ugenini lakini inasikitisha kuwa hilo halikufanyika. Hata hivyo wameridhika na matokeo hayo wakati wakiangazia macho yao kwa mechi ya marudio.

Kocha wa Borussia Dortmund Jurgen Klopp ameelezea kuridhika kwake kutokana na sare hiyo lakini akawaonya wachezaji wake kutofikiria kuwa tayari wana tikiti ya kucheza nusu fainali…

Mkufunzi wa BVB Dortmund Jurgen Klopp hakutarajiwa mambo kuwa rahisi Uhispania
Mkufunzi wa BVB Dortmund Jurgen Klopp hakutarajiwa mambo kuwa rahisi UhispaniaPicha: Bongarts/Getty Images

Amesema siyo rahisi kuwaondoa Malaga katika mkondo wao na hiyo ndio hatari kubwa. Lakini walimudu kupata matokeo mazuri dhidi ya mpinzani aliyejiandaa vyema ambaye hakutishika na nafasi za Dortmund za kufunga magoli, na badala yake akaendekea kushambulia.

Ronaldo awaongoza Madrid kwa ushindi

Katika mchuwano mwingine wa jana usiku, Real Madrid ni kama tayari wamejikatia kibali cha kucheza katika nusu fainali, baada ya kupata ushindi wa mabao matatu kwa sifuri dhidi ya Galatasaray.

Vijana hao wa mkufunzi Jose Mourinho walikuwa moto wa kuotea mbali wakati Cristiano Ronaldo akifungua ukurasa wa magoli katika dakika ya tisa.

Real Madrid waliwazidi maarifa mabingwa wa Uturuki Galatasaray katika uga wa Santiago Bernabeu
Real Madrid waliwazidi maarifa mabingwa wa Uturuki Galatasaray katika uga wa Santiago BernabeuPicha: picture-alliance/dpa

Goli la Karim Benzema lilidhihirisha ni kwa ni Mourinho alimchagua katika kikosi cha kumi na mmoja wa kwanza..kisha nguvu mpya Gonzalo Higuain akafanya mambo kuwa matatu bila jibu, na kuhitimisha kibarua cha mkondo wa kwanza.

Kikosi cha Galatasaray kilichokuwa na washindi wa zamani wa champions League, na wachezaji wa Mourinho, Didier Drogba na Wesley Sneijder pamoja na mshambuliaji aliye katika hali nzuri Burak Yilmaz, hakikufanya chochote cha kuwarihidha mashambiki wake waliosafiri wka wingi katika uwanja wa Santiago Bernabeu.

Mourinho amewasifu wachezaji wake kwa kuonyesha ukakamavu na mchezo mzuri baada ya ushindi huo. Amesema walijiandaa vyema kwa mchuwano huo na hivyo walifanya mashambulzii na wakati huo huo wakiweka ulinzi mkali. Mourinho ameongeza kuwa kibarua bado hakijakamilika.

Naye kocha wa Galatasaray Fatih Terim amekiri kuwa timu yake iliadhibiwa kutokana na makosa madogo na akamnyoshea kidole refarii. Anasema refa alishindwa kuona makosa kama vile tukio la Sergio Ramos wa Real Madrid kukanyaga kwa nguvu kiatu cha mchezaji Yilmaz katika kijisanduku.

Mwandishi: Bruce Amani/AP

Mhariri Josephat Charo