1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoUingereza

Manchester United yaibana mbavu Liverpool

6 Januari 2025

Katika Ligi ya Premier ya England, Manchester United imeipunguza kasi ya mbio za ubingwa baada ya kuibana Liverpool kwa sare ya 2-2 katika mechi ya kukata na shoka.

https://p.dw.com/p/4org0
Kocha wa Liverpool Arne Slot
Liverpool chini ya kocha Mholanzi Arne Slot wanapigiwa upatu kubeba ubingwa wa Ligi ya Premier EnglandPicha: Propaganda Photo/Imago Images

Katika Ligi ya Premier ya England, Manchester United imeipunguza kasi ya mbio za ubingwa baada ya kuibana Liverpool kwa sare ya 2-2 katika mechi ya kukata na shoka. Sare hiyo iliwapandisha Utd hadi nafasi ya 13, lakini bado wako nyuma ya nambari sita Man City na pengo la pointi 11 na 13 nyuma ya nambari nne Chelsea.

Lakini sare hiyo iliwafurahisha mashabiki wa Utd waliomudu baridi kali na theluji kusafiri Kwenda Liverpool. Ruben Amorim ni kocha wa United. "Nadhani ni dalili nzuri sana, ni wazi kabisa. Tumepoteza mechi tatu mfululizo nyumbani. Baadhi ya mechi hizo tulifungwa mabao mawili bila ya kufanya chochote. Kwa hiyo leo nimekasirika, nimekasirika sana. Nimefurahishwa na matokeo lakini kila mtu leo ​​ataiambia timu kwamba walifanya kazi nzuri. Leo nimeruhusiwa kuwa mtu pekee aliyekasirishwa na timu, lakini leo tulicheza kama timu."

Liverpool iliimaliza wikiendi pale pale ilipoanzia – na uongozi wa pengo la pointi sita dhidi ya Arsenal kileleni. Huyu hapa kocha wa Liverpool Arne Slot "Bila shaka, kwetu ni kama tumeangusha pointi mbili. Nadhani kwa watu wengi, kile kinachokaa kichwani mwao zaidi na kwa muda mrefu ndicho kilichotokea mwishoni. Na hiyo ilikuwa nafasi kubwa kwa Maguire, bila shaka. Lakini unachosahau ni kwamba dakika mbili kabla ya nafasi yake, Virgil van Dijk labda alikuwa na nafasi kubwa ya kufanya tushinde 3-2. Mwishowe, ulikuwa mchezo mgumu."

Ilitarajiwa kuwa The Gunners wangewawekea Liverpool shinikizo lakini watajutia kuangusha pointi baada ya sare ya 1-1 dhidi ya Brighton huku Chelsea sasa wakiwa bila ushindi katika mechi nne mfululizo.

afp, reuters