Mandela bado alazwa Hospitali
25 Desemba 2012Maelfu ya waafrika kusini wamemuombea kiongozi mkongwe wa nchi hiyo Nelson Mandela anayeendelea kulazwa Hospitali.Taarifa zilizotolewa na rais Jacob Zuma aliyemtembelea hospitali katika sikukuu ya Krismasi kiongozi huyo aliyepigana dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini,zimesema anaendelea vyema na kwamba madaktari wameridhishwa na maendeleo ya afya yake.
Mandela mashindi wa tuzo ya amani ya Nobel mwenye umri wa miaka 94 amekuwa hospitali mjini Pretoria kwa zaidi ya wiki mbili baada ya kulazwa kwa ajili ya uchunguzi wa kawaida wa kiafya.Baadae alifanyiwa upasuaji wa kuondosha uvimbe kwenye nyongo.
Kiongozi huyo wa kwanza Muafrika aliyechaguliwa kwa njia ya Kidemokrasia nchini Afrika Kusini katika uchaguzi wa kihistoria mwaka 1994,baada ya miongo ya mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi,bado amebakia kuwa alama ya mapambano dhidi ya ubaguzi na vitendo visivyokuwa vya haki nyumbani Afrika Kusini na duniani kwa ujumla.
Kiongozi huyo wa zamani wa Afrika Kusini ana historia ya matatizo ya mapafu tangu wakati alipopata maradhi ya kifua kikuu alipokuwa jela kama mfungwa wa kisiasa,lakini hii ni mara ya kwanza kulazwa hospitali kwa muda mrefu zaidi tangu alipoachiwa huru mwaka 1990.
Itakumbukwa kwamba mwaka 2011 alilazwa hospitali mjini Johannesberg akiwa na matatizo ya kupumua na mwezi Februari mwaka huu akalazwa tena kutokana na matatizo ya maumivu ya tumbo ingawa aliruhusiwa kwenda nyumbani siku ya pili baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu na kuonekana kwamba hana matatizo makubwa.
Wiki iliyopita Rais Jacob Zuma aliyechaguliwa tena kuwa rais wa chama tawala nchini humo cha National Congress,ANC aliielezea hali ya kiongozi huyo wa zamani kuwa mbaya,akisema kwamba familia yake inashukuru mchango wa umma katika kumuuguza Mandela.
Lakini hadi wakati huu taarifa zinazotoka ofisi ya Rais Zuma zinasisitiza kwamba Mzee Madiba yuko katika hali nzuri ingawa hakuna tarehe iliyotajwa ya kuruhusiwa kwake kutoka hospitali.Mkongwe huyo wa kisiasa alikaa gerezani miaka 27 na baada ya kuachiwa huru alitumia umaarufu wake kutia msukumo maridhiano kati ya wazungu na waafrika weusi,Na maridhiano hayo ndiyo yakawa chachu ya kuundwa taifa hilo la mchangayiko wa watu.
Mandela aliapishwa kuwa rais wa kwanza mweusi nchini Afrika Kusini mwaka 1994,na akaachia madaraka mwaka 1999 baada ya kuongoza kwa muhula mmoja.Amejiepusha kuonekana katika mikusanyiko ya umma kwa muda wa muongo mmoja sasa kutokana na afya yake,lakini ameendelea kutembelewa nyumbani kwake na watu mashuhuri wa ndani na wa Kimataifa,akiwemo rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton aliyemtembelea mwezi Julai.
Mwandishi Saumu Yusuf
Mhariri Mohamed Dahman