Serikali yaahidi msaada zaidi
25 Septemba 2015Kwa muda wa saa kadhaa serikali ya shirikisho na zile za majimbo zimekutana katika mkutano maalum jana jioni, wakijadili kuhusu msaada wa kifedha. Hakukuwa na shutuma kubwa zilizojitokeza katika mkutano huo. Isipokuwa tu taratibu na kwa shingo upande waziri wa fedha wa serikali ya shirikisho alikubali madai yaliyotolewa.
Si rahisi kutoa euro bilioni 2 na kisha hadi euro bilioni 4 nyingine mwaka ujao , kwa ajili ya kuwapatia wakimbizi huduma za uhakika, kwasababu pamoja na fedha hizo , kuna gharama nyingine za kuwasafirisha wahamiaji kwenda katika maeneo waliyotengewa.
Malipo kwa wakimbizi
Malipo ya euro 670 kila mwezi kwa kila mkimbizi ni mwanzo tu. Msaada wa awali katika nyakati hizi za mzozo, ambamo kila siku maelfu ya wakimbizi wanaingia nchini Ujerumani na ikitiliwa maana kwamba siku za majira ya baridi zinasogea karibu na wakimbizi wanatakiwa kupatiwa huduma muhimu haraka.
Hilo pekee ni tatizo, kama vile wafanyakazi wa wizara ya afya na jamii mjini Berlin wanavyoliona.
Hatua itakayochukua takriban siku tatu , na baada ya hapo wakimbizi kwa kiasi fulani watapaswa kuwa wavumilivu, hadi pale msitari mrefu wa kuandikishwa utakapomalizika.
Kwa hivi sasa fedha zinahitajika , ili kuweza kupunguza matafaruku huu uliopo pamoja na kupatikana treni zitakazowapeleka wakimbizi wanakostahili kuishi. Lakini hadi sasa hilo halijafanyika. Watahitajika waalimu, wataalamu wa saikolojia na wafanyakazi wengi tu wa huduma za jamii.
Watoto watalazimika kuingizwa katika shule za chekechea pamoja na wengine kuingia katika shule za kawaida, watu wazima watalazimika kupatiwa masomo ya lugha, pamoja na mafunzo ya kazi.
Kuna mahitaji ya nyumba
Kuna ulazima wa kujenga nyumba zaidi, kwa kuwa serikali kuu itatumia kiasi cha euro milioni 500 ili kuchochea ujenzi wa nyumba hizo.
Na pamoja na hayo serikali za majimbo na mitaa zinahitaji wafanyakazi zaidi, ili kuweza kuwahudumia vizuri zaidi wakimbizi hao, ambao bado wanaendelea kuja, kama hali inavyoonekana sasa.
Bado halmashauri ya Umoja wa Ulaya inakadiria kwamba watu watakaoomba hifadhi watafikia milioni tano katika muda wa miaka mitatu ijayo. Hata wakati huu ambapo sheria ya uhamiaji imeimarishwa zaidi na wakimbizi wengi kukataliwa, bado wakimbizi 500,000 watabakia nchini Ujerumani. Kuwajumuisha katika jamii itakuwa kibarua kigumu mno na kugharimu fedha nyingi.
Fedha zinapaswa kupatikana kutoka serikali kuu, kwasababu serikali za majimbo na za mitaa zimekuwa kwa miaka mingi zikitumika kutoa huduma kama hizo na hazina uwezo huo kwa sasa.
Ni suala la kitaifa na serikali kuu ina uwezo wa kubeba mzigo huo.
Mwandishi: Sabine Kinkartz / ZR / Sekione Kitojo
Mhariri : Idd Ssessanga