1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Tshisekedi anakabiliwa na changamoto gani?

25 Januari 2019

Baada ya ushindi wa uchaguzi uliozusha mabishano katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Felix Tshisekedi anakuwa rais mpya wa nchi hiyo ya Afrika ya Kati.

https://p.dw.com/p/3C6il
Kongo Felix Tshisekedi
Picha: picture-alliance/dpa/B. Curtis

Kwa mujibu wa uhariri wa Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya DW, Andrea Schmidt, halitokuwa jukumu rahisi ikizingatiwa kwamba ushindi huo ameupata kutokana na msaada wa utawala wa rais wa zamani Joseph Kabila.

Habari za kufurahisha ni kwamba kwa mara ya kwanza katiba historia ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, zoezi la kukabidhi madaraka linafanyika kwa njia ya amani. Hata hivyo lina ila zake.

Raisi mpya Felix Tshisekedi japo kama anajivunia uungaji mkono wa chama kikuu cha upinzani UDPS-Umoja kwa ajili ya Demokrasia na Maendeleo ya Kijamii, hata hivyo wachunguzi wengi wanaamini ushindi wake ameupata kutokana na visa vya udanganyifu na ushawishi wa utawala usiopendwa wa Kabila.

Fayulu mpinzani mkuu wa Tshisekedi

Mpinzani wake mkubwa katika uchaguzi wa Desemba 30, 2018 Martin Fayulu wa kutoka katika muungano wa upinzani wa Lamuka, kwa mujibu wa ripoti kutoka vituo vya kupiga kura, amejipatia zaidi ya asilimia 60 ya kura.

Wakongomani wamevunjwa moyo na uchaguzi wa hadaa ya kidemokrasia katika nchi yao, hata hivyo ni wachache tu wanaounga mkono wito wa maandamano alioutoa Fayulu. Wanataka hatimae kuona maendeleo, umoja na amani baada ya miongo kadhaa ya mizozo.

Wamechoshwa kuona walioko serikalini wakizidi kutajirika na wakati huo huo, watoto wadogo wakifa kwa maradhi ya kipindupindu, watu wakisumbuliwa na njaa, wakilazimika kuwakimbia wanamgambo, wanawake kubakwa kwa wingi miundo mbinu hakuna na hali ya ukosefu wa ajira ikizidi kuenea.

DW Kiswahili | Andrea Schmidt
Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya DW, Andrea SchmidtPicha: DW/L. Richardson

Wanataka kuachana na mitindo ya mwenye nguvu mpishe na asiyejimudu azidi kutaabika. Mnamo miaka inayokuja Tshisekedi atabidi adhihirishe kwamba yeye si kikaragosi cha Kabila. Mwanasiasa huyo mwenye mri wa miaka 55 inabidi adhihirishe, licha ya kwamba uchaguzi haukuwa wa haki wala wa uwazi, anataka kuwa rais wa Wakongomani wote.

Chama cha Kabila kinadhibiti wingi wa viti bungeni

Haitakuwa rahisi kwa sababu chama cha Kabila PPRD, chama cha wananchi kwa ajili ya kurejesha demokrasia ndicho kinachodhibiti wingi wa viti katika bunge na kitataka kumtia kishindo Tshisekedi afuate kile ambacho pengine kilizungumzwa kwa siri.

Lakini mfano wa Angola umebainisha kwamba raisi mpya mfano wa Joao Lourenco aliyekuja madarakani kutokana na ridhaa ya utawala wa zamani wa Dos Santos amefanikiwa kulazimisha mfumo wake mwenyewe na kupambana na muondo wa zamani ulioota mizizi.

Hata hivyo, haitakuwa kazi rahisi katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo yenye wakaazi milioni 80 na makundi dazeni kadhaa ya waasi wanaobidi kupatiwa ufumbuzi, pamoja na shughuli za kilimo zinazohitaji kuendelezwa. Seuze tena zoezi la kukabidhi madaraka limefuatia udanganyifu katika vituo vya kupigia kura.

Tshisekledi anabidi ajaribu kuwajumuisha serikalini wafuasi wa muungano wa upande wa upinzani Lamuka unaowaleta pamoja miongoni mwa wengine, wanasiasa mashuhuri akina Jean Pierre Bemba na Moise Katumbi anaeishi uhamishoni. Hiyo ndio hali pekee itakayosaidia kuleta amani ya kweli katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Mwandishi:Schmidt Andrea/Hamidou Oummilkheir
Mhariri: Josephat Charo