1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uamuzi wa Mahakama ya Kenya uzae marekebisho

Andrea Schmidt
1 Septemba 2017

Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya DW, Andrea Schmidt, anasema baada ya Mahakama ya Juu ya Kenya kuufuta uchaguzi na kuamuru mwengine, sasa ni wakati wa Kenya kuendelea kuonesha njia kwa kuheshimu maamuzi hayo na kurekebisha.

https://p.dw.com/p/2jE1p
KENIA-NAIROBI- Wahlen Hand wird markiert
Picha: picture-alliance/Photoshot/M. Chenguang

Huu ni ushindi wa wazi kwa demokrasia barani Afrika. Kwa mara ya kwanza Mahakama ya Juu nchini Kenya imeyatangaza matokeo ya uchaguzi uliokwishamalizika kuwa ni batili, baada ya upinzani ukiongozwa na kinara wao, Raila Odinga, kuyawekea pingamizi mahakamani, na hatimaye kufanikiwa kupata haki. 

Baada ya matokeo yaliyotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kumpa Uhuru Kenyatta ushindi wa asilimia 54.27 na kumuwacha nyuma Odinga kwa asilimia 44,74, kiongozi huyo wa upinzani aliamua kufanya kile ambacho ni mzoefu nacho - kupinga matokeo na kwenda mahakamani.

Hata hivyo, uamuzi wa mara hii wa Mahakama ya Juu chini ya Jaji Mkuu David Maranga haukuwa umefikiriwa na wengi. Kwa kutumia uzoefu wa mwaka 2013, ambapo Odinga aliwasilisha zuio kama hili, wengi walidhani kuwa na mara hii pia angelishindwa. 

Lakini tangu Jumatatu ilipoiamuru IEBC kuwapa wapinzani fursa ya kuona mitambo ya kukusanyia matokeo ya tume hiyo, kila mtu alianza kuona kuwa sasa inakusudia kuwa kweli madhubuti. Inaonesha kuwa idara ya mahakama nchini Kenya inaichukulia kazi yake kwa umakini, iko huru na haina khofu mbele ya vyombo vya dola.

Funzo kwa Afrika nzima

Schmidt Andrea
Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya DW, Andrea Schmidt

Vile vile, maoni kutoka kwa raia wa mataifa jirani kuhusiana na uamuzi huu wa mahakama ya juu yanatia moyo. Hawa ni raia ambao wenyewe ni wahanga wa usaliti unaofanywa na dola dhidi ya kura zao.

Uamuzi huu wa leo, kwa hivyo, unatoa matumaini kwa chaguzi zijazo sio tu nchini Kenya, bali pia katika eneo zima la Afrika Mashariki na Kati na Ukanda wa Maziwa Makuu.

Funzo kubwa ni kuwa si kila mara aliye madarakani ndiye mwenye uamuzi wa mwisho kwa kila jambo. 

Uhuru Kenyatta kwa upande wake ameamua kuonesha tafauti. Licha ya kwamba hakupendezwa na maamuzi haya ya Mahakama ya Juu, lakini ametangaza waziwazi kuwa anayakubali.

Sasa marekebisho makubwa yafanyike

Hata hivyo, ishara hizi njema kwa demokrasia ya Kenya hazipaswi kuishia hapo tu. Mahakama ya Juu imeamuru uchaguzi mpya kufanyika ndani ya siku 60 kutoka sasa.

Lakini, kwa vyovyote vile, haielekei kuwa uchaguzi huo uandaliwe na kusimamiwa na chombo kile kile ambacho kimehusika na uchaguzi uliofutwa.

Kwa Wakenya wengi, IEBC haiaminiki tena. 

Tayari baadhi ya Wakenya wanashauri kuwa ili uchaguzi mwengine uwe wa kuaminika, basi unapaswa kusimamiwa na Umoja wa Mataifa.

Lakini mimi naona waende mbali zaidi ya hapo. Kwanza, serikali iliyopo sasa madarakani ikae kitako na upinzani kuteua tume mpya ya uchaguzi. Pili, yale mapungufu yote ya uchaguzi uliofutwa yajuilikane na yawekwe wazi kabla ya uchaguzi mpya ndani ya miezi miwili hii.

Pia waangalizi wa kimataifa waliupa sifa uchaguzi wa Agosti 8 kuwa ulikuwa huru na wa haki. Sasa wanapaswa kujifikiria upya. 

Jengine kubwa pia kwa muhimu ni kwa wafuasi wa chama tawala Jubilee kufanya kama alivyofanya kiongozi wao, Rais Uhuru Kenyatta, kuyakubali maamuzi ya mahakama. 

Wakenya wanastahiki uchaguzi wa kweli.

Mwandishi: Andrea Schmidt
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Iddi Ssessanga