Maoni: Ujerumani yahitaji masharti sawa kujikinga na corona
27 Agosti 2020Mara nyingi watu wanasema Wajerumani wana nidhamu na waangalifu. Wanasema ndiyo maana nchi yetu ilifanikiwa kupambana vizuri na wimbi la kwanza la virusi vya corona. Lakini hiyo ilikuwa zamani.
Mtu yeyote ambaye yuko Ujerumani leo anashuhudia kukosekana kwa nidhamu, kutokuwa na uhakika na wakati mwingine hata ukosefu wa usalama linapokuja suala la maamuzi ya kisiasa yanayotolewa.
Sheria za kiholela za kuvaa barakoa, na kuzuia hafla
Kwa mfano kwenye jimbo la Berlin, shughuli zinazowahusisha zaidi ya watu 500 zinaruhusiwa, huku kwenye jimbo jirani la Brandenburg wanaruhusiwa kuwa na hadi watu 1,000.
Katika jimbo la magharibi lenye watu wengi zaidi nchini Ujerumani, North Rhine-Westphalia, shule zinawataka wanafunzi kuvaa barakoa muda wote – wakiwa darasani, kwenye varanda, kwenye uwanja wa michezo au kwenye mazingira ya shule.
Lakini kwa upande wa Berlin mambo sio magumu hivyo na wanafunzi hawahitaji kuvaa barakoa wakiwa darasani. Suala la hiari linazingatiwa.
Hivyo, ni upi msingi wa kufanya maamuzi ya kujikinga na virusi vya corona? Je, kila mwanasiasa ana wataalamu wake ambao hutathmini hali ya hatari tofauti? Hali hii yote imesababisha mkanganyiko miongoni mwa wananchi wa Ujerumani.
Na sasa idadi ya watu walioambukizwa virusi vya corona nchini Ujerumani imeongezeka tena. Wengi wa wale wanaoumwa sasa, waliambukizwa wakati wakiwa kwenye likizo ya majira ya joto nje ya nchi.
Hivyo, swali ni je: Kwa nini upimaji wa lazima kwa wale wanaorejea kutoka kwenye maeneo yenye hatari kubwa ulianzishwa wakati nusu ya Wajerumani walikuwa wamesharejea tayari kutoka likizo?
Na kama niko kwenye uwanja wa ndege, ni nini maana ya kukaa umbali wa mita 1.5 kutoka kwa mtu mwingine, wakati ndani ya ndege iliyojaa watu naketi karibu na jirani yangu? Kwa nini watu wachache tu ndiyo wanaruhusiwa ndani ya mkahawa, lakini sio ndani ya maduka makubwa?
Masharti sawa yanahitajika nchi nzima
Mkanganyiko wote huu wa hatua za kujikinga na virusi vya corona umesababisha watu zaidi na zaidi kuipuuza miongozo ya usalama iliyowekwa. Hivi sasa watu wanafanya tena sherehe kama vile hapakuwa na virusi vya corona, au vilikuja na kuondoka.
Mambo hayawezi kuendelea hivi. Tunahitaji hatua zilizo wazi na ambazo ziko sawa kwa Ujerumani yote. Tunahitaji nidhamu na mshikamano katika jamii na wanasiasa ambao hawautumii mzozo wa virusi vya corona kama njia ya kuendeleza zaidi kazi zao na wasifu wao, lakini badala yake wanaungana pamoja kwa usalama na faida ya kila mmoja.