1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazeti

Abdu Said Mtullya2 Aprili 2013

Wahariri wanazungumzia juu ya ushindi wa masikini wa dunia kufuatia uamuzi wa mahakama nchini India.Na pia wanatoa maoni juu ya machachari ya hatari ya kiongozi wa Korea ya kaskazini.

https://p.dw.com/p/1884H
Kampuni ya dawa Novartis ya Uswisi
Kampuni ya dawa Novartis ya UswisiPicha: picture alliance/AP Photo

Gazeti la "Donuakurier"linatoa maoni juu ya uamuzi wa Mahakama ya nchini  India kuikatalia kampuni ya dawa ya Uswisi,Novartis hati miliki ya dawa ya saratani ya bei nafuu. Mhariri wa gazeti hilo anasema uamuzi huo ni sahihi na wa haki.

Anaeleza kuwa Kampuni ya Novartis haikuwa na lengo la kupata hati miliki kwa ajili ya kutengeneza dawa ya aina mpya.Lengo lake lilikuwa kuifanyia mabadiliko tu dawa ile ile ya zamani na kuiuza tena kama mpya kwa kutumia hati miliki mpya. Hukumu iliyotolewa na mahakama ya India ni ushindi ulioleta uzima nchini India

Naye mhariri wa gazeti la "Reutlinger General-Anzeiger"anatilia maanani
kwamba dawa za bei nafuu zinahitajika katika juhudi za kupambana na maradhi kama saratani ,ukimwi, kifua kikuu na malaria.Hukumu iliyotolewa na mahakama ya nchini India ni ushindi,siyo nchini India tu bali pia katika nchi nyingine,ikiwa pamoja na Ujerumani.

Machachari ya Kim Jong-Un

Gazeti la "Bild Zeitung" linayazungumzia machachari ya  hatari ya kiongozi wa Korea ya Kaskazini. Katika muda wa siku kadhaa, Korea ya Kaskazini imekuwa inatoa vitisho vya kuzishambulia ,Korea ya Kusini na Marekani.

Mhariri wa"Bild-Zeitung"ansema kiongozi huyo,Kim Jong-Un anafanya kama wanavyofanya madikteta wengine wote, pale wanaposhindwa kuwapa watu wao chakula cha kutosha.Hata hivyo mivutano ya kijeshi inaiathiri dunia yote kiuchumi. Mhariri huyo anesema jambo moja linapasa kuwa wazi, kwamba ikiwa Korea ya kaskazini, itaruhusiwa kuendelea na mipango yake ya silaha za nyuklia, basi huo utakuwa mwaliko kwa madikteta wa Iran na Syria.

Mhariri wa "Augsburger Allgemeine"anauliza jee ni kweli Kim Jong Un anataka vita au anacheza mchezo wa mazingaombwe tu?

Mhariri huyo anaeleza;kwanza kabisa Korea ya Kaskazini haina tekinolojia ya  kuiwezesha kuazisha vita vya kiatomiki na Marekani.Jambo la pili,anaposema kuwa nchi yake imo katika hali ya hatari ya vita na jirani yake, hilo siyo tangazo jipya.Ukweli ni kwamba baada ya kumalizika kwa vita vya Korea mnamo mwaka wa 1953,nchi mbili za Korea zilifikia mapatano ya kusimamisha mapambano tu.

Jambo jingine ni kwamba kuanzisha vita dhidi ya Marekani kutakuwa na maana ya utawala wa Korea ya kaskazini kujipalia makaa kama pweza. Machachari ya kiongozi wa Korea ya kaskazini Kim Jong Un yanaweza kuonekana dhahiri hata na wale wasioona. Yeye ni kifauwongo tu!

Mwandishi:Mtullya  Abdu /Deutsche Zeitungen:

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman