Umoja wa Ulaya usikubali Wakurdi wakandamizwe
6 Oktoba 2015Gazeti la "Flensburger Tageblatt" linatilia maanani kwamba Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amefanya ziara kwenye makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels ili kuuzungumzia mgogoro wa wakimbizi.
Mhariri wa gazeti hilo anasema ni muhimu kuipa Uturuki msaada kwa sababu hali katika kambi za wakimbizi,wanaotoka Syria ni ya maafa ,nchini Uturuki. Hata hivyo pana haja ya kuwapo uangalifu. Umoja wa Ulaya asilani usikubali msimamo mkali wa Uturuki dhidi ya Wakurdi, ati kwa sababu Uturuki, inawadhibiti wakimbizi wanaoingia Ulaya.
Gazeti la "Rheipfalz" linazungumzia juu ya ziara ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel nchini India lakini kwa kuyatathmini aliyofanya Waziri Mkuu wa nchi hiyo , Narendra Modi tangu aingine madarakani.
Mhariri huyo anasema Waziri Mkuu Modi alichaguliwa mwaka jana ,na aliingia madarakani kwa kishindo kwa sababu watu wa India walikuwa na imani kubwa , kwamba angelileta mabadiliko.
Waziri Mkuu Modi aliahidi kutenga mamilioni ya nafasi za ajira na kuondoa umasikini nchini India.Ni kweli kwamba aliweza kuleta ustawi mkubwa katika jimbo lake la uzawa la Gujarat, lenye watu milioni 60. Lakini gazeti linasema , kuhusu India kwa jumla,Waziri Mkuu Modi yuko mbali sana na yale aliyoahidi.
Dawa ya kutibu malaria itaokoa maisha ya wengi
Mhariri wa "Nürnberger Nachrichten" anatilia maanani umuhimu wa dawa ya malaria iliyogunduliwa na madaktari waliopewa tuzo ya Nobel katika tiba. Mhariri huyo anaeleza kwamba nchi nyingi zinazoendelea hazina fedha kwa ajili ya kuendeshea kampeni kabambe juu ya kuepuka njia zinazoeneza maradhi.
Anasema nchi hizo pia hazina fedha za kutosha kwa ajili ya kuweka taratibu za kinga za maradhi. Ndiyo sababu kwamba dawa iliyogunduliwa na madaktari watatu waliopewa tuzo ya Nobel inapaswa kutiliwa maanani.
Mhariri wa "Nürnberger Nachrichten" anasema ugunduzi huo ni muhimu kwa sababu siyo wengi, duniani wanaojali juu ya ugonjwa wa malaria ambao aghalabu huwakumba masikini.
Gazeti la "Neue Presse" linasema mpango wa Shirika la ushirikiano wa kiuchumi na mandeleo OECD juu ya kupambana na wahalifu wanaokwepa kulipa kodi ni wa kihistoria.
Gazeti hilo linafahamisha kwamba serikali zinapoteza dola hadi Bilioni 240 duniani kote kila mwaka kutokana na uhalifu wa makampuni hayo. Hata hivyo mhariri wa gazeti hilo anatahdahrisha kwamba hadi utakapofika wakati wa kuutekeleza mpango huo, wahalifu watakuwa tayari wameshaupata ujanja mwingine wa kuwawezsha kukwepa kulipa kodi.
Mwandishi:Mtullya abdu/Deutsche Zeitungen.
Mhariri: Abdul-Rahman