Maoni ya wahariri
13 Desemba 2012Juu ya mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya, mhariri wa gazeti la "Tagespost" analalamika kwamba ,jambo muhimu kabisa linakosekana.Mhariri huyo anaeleza kuwa juhudi za kukabiliana na mgogoro wa madeni, zinasababisha mogoro mwingine: hakuna imani. Anasema siyo sarafu ya Euro iliyoshindwa au mradi wa Umoja wa Ulaya, bali ni nchi ndizo zilizoshindwa.Na kwa hivyo matatizo ambayo hayawezi kutatuliwa katika ngazi ya kitaifa yashughulikiwe katika ngazi ya kijumuia.
Gazeti la "Reutlinger General -Anzeiger" linatoa maoni juu ya hatua ya Korea ya Kaskazini ya kurusha roketi, licha ya malalamiko ya nchi jirani na nyingine kadhaa. Mhariri wa gazeti hilo anasema Korea ya Kaskazini inarusha roketi angani, badala ya kuoka mikate. Hatahivyo aneeleza kuwa inapasa kutilia maanani kwamba kiongozi wa nchi hiyo,Kim Jong Un aliekirithi kiti cha baba yake analitegemea sana jeshi. Kwa hivyo shutuma za Umoja wa Mataifa na vitisho vya Umoja wa Ulaya kuweka vikwazo havitamshtua kiongozi huyo.
Bunge la Ujerumani limeupitisha mswada wa sheria juu ya kuwapa wazazi wa kiyahudi na wa Kiislamu msingi wa kisheria wa kuendelea kuwatahiri watoto wao. Lakini mhariri wa gazeti la "Donaukurier" anasema bado yapo maswali mengi yanayopaswa kuulizwa.Mhariri huyo anaeleza kwamba mambo matatu yanapaswa kuangaliwa,afya ya mtoto,wajibu wa wazazi na haki ya uhuru wa kuabudu.
Sheria hubadilika kutegemea na mabadiliko ya jamii.Ndiyo sababu wakati wote itapasa kuuliza maswali juu ya sheria hiyo. Serikali ya Ujerumani haikuitumia fursa hiyo, na sasa imesalimu amri mbele ya mashinikizo ya jumuiya za kidini. Na mhariri wa "Sudwest Presse" anasema, kinachohitajika sasa ni mageuzi kutokea ndani. Sheria iliyopitishwa haina maana kwamba maumivu anayoyapata mtoto wakati wa kutahiriwa yameondoka. Hilo ni muhimu kulitambua. Anasema mageuzi ya kanuni za kidini yanapaswa kufanyika kutokea ndani ya jumuiya za kidini.Ni kwa kiasi gani jambo hilo linaweza kufanyika itategemea na uamuzi na imani ya dini husika.
Mwandishi:Mtullya abdu/Deustche Zeitungen.
Mhariri: Yusuf Saumu