Maoni ya walimwengu kuelekea mkuu mpya wa IMF
29 Juni 2011Christine Lagarde,mwanamke wa kwanza kuongoza shirika hilo la fedha la kimataifa,baada ya wadhifa huo kushikiliwa na wakuu 10 wa jinsia ya kiume,ataanzaa shughuli zake July 5 ijayo.
Atakamata nafasi ya mfaransa mwenzake Domoniique Strauss-Kahn aliyelazimika kujiuzulu mwezi May uliopita baada ya kushitakiwa kwa madai ya kumbaka mtumishi wa hoteli moja mjini New-York.
Katika taarifa yake bibi Christine Lagarde ametilia mkazo jukumu la shirika la IMF akisema ni jukumu la kudumu ,la maana na la haki ,ili kukahikisha ukuaji mkubwa wa kiuchumi na wa kudumu pamoja na kudhamini hali bora ya maisha kwa wote.
Kabla ya kuchaguliwa kuliongoza shirika la fedha la kimataifa bibi Christine Lagarde alisema:
"Mie si mgombea wa Ulaya na wala si mgombea wa Ufaransa,mie ni mgombea wa mataifa yote 187 wanachama wa shirika hili la kimataifa."
Mara baada ya kuchaguliwa,ikulu ya Ufaransa Elysee imempongeza na kusema kuchaguliwa kwake ni "ushindi kwa Ufaransa."
Nchini Marekani waziri wa fedha Timothy Geithner amesifu "kipaji cha aina pekee na maarifa aliyp nayo mwanasiasa huyo wa Ufaransa.
Waziri wa fedha wa India Pranab Mukhrejee amesema kwa upande wake nchi yake imeunga mkono kuchaguliwa bibi Christine Lagarde kuwa mkuu wa shirika la fedha la kimataifa kwasababu inataka kuchangia katika utaratibu wa kusaka ridhaa anaopanga kuufuata waziri wa uchumi na fedha wa Ufaransa.
Waziri mwenzake wa Brazil Guido Mantega amesema nchi yake imemuunga mkono bibi Lagarde kwasababu ameahidi kutilia maanani zaidi matakwa ya mataifa yanayoinukia kiuchumi.
Arvind Subramanian wa taasisi ya Peterson mjini Washington anahisi nchi zinazoinukia kiuchumi zimeitupa fursa ya kushinikiza mageuzi katika shirika la fedha la kimataifa kwa kutomuunga mkono mgombea wa kutoka Mexico Agustin Carstens au kwa kuwakilishwa na mgombea waliomchagua wenyewe.
Mashirika yasiyomilikiwa na serikali yamekosoa vikali kuchaguliwa bibi Lagarde kuongoza shirika la fedha la kimataifa IMF.
"Kiini macho katika utaratibu wa kuchaguliwa mkuu wa shirika la IMF kinachafua imani ya walimwengu kwa shirika hilo"-limesema shirika la OXFAM kataika taarifa yake.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP
Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed