1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maonyesho ya historia ya Tanzania yazinduliwa Berlin

Sylvia Mwehozi
3 Desemba 2024

Maonyesho kuhusu historia ya Tanzania yamezinduliwa mjini Berlin Ujerumani, kwa lengo la kuelezea historia tata ya kale ya jamii za watu walioishi katika nchi ambayo sasa ni Tanzania.

https://p.dw.com/p/4nflQ
Maonyesho kuhusu historia ya Tanzania-Berlin
Maonyesho kuhusu historia ya Tanzania yaliyofanyika BerlinPicha: Sylvia Mwehozi/DW

Tanzania na Ujerumani zimekuwa na historia kubwa inayoanzia enzi za ukoloni wakati ilipokuwa sehemu ya koloni la wajerumani na kufahamika kama "Ujerumani ya Afrika Mashariki."

Historia hiyo hata hivyo imejaa machungu kutokana na alama ya ukoloni iliyoachwa na Wajerumani waliowakandamiza wenyeji na kuwatesa wakati wa utawala wao.

Soma pia: Ujerumani yawaomba radhi Watanzania kwa madhila ya Ukoloni

Miongoni mwa masuala ambayo hadi sasa yanaendelea kuibua mijadala ni wizi wa vitu au mali za kitamaduni zilizoporwa na Wajerumani kutoka jamii za wazawa ikiwemo pia mabaki ya miili ya viongozi wa kimila.

Chifu Emmanuel Xavier Zulu Gama
Chifu Emmanuel Xavier Zulu Gama wa kwanza ni kiongozi wa jamii wa wangoni kutoka songea Tanzania.Picha: Sylvia Mwehozi/DW

Katika maonyesho haya timu ya wahifadhi kutoka Ujerumani, Berlin na Songea walishirikiana na ndugu za jamii ambazo vitu vyao viliporwa kuzungumzia umuhimu wa kazi hizo katika jamii yao ya sasa.

Flower Manase Msuya ni mtafiti kutoka Makumbusho ya taifa Tanzania ambaye ameshiriki kuandaa maonyesho haya. "Maonyesho haya sana yanhusu historia ya Tanzania kabla na wakati wa ukoloni na yanahusisha zaidi vifaa ambavyo vilichukuliwa kipindi cha ukoloni wa Kijerumani katika eneo la Afrika Mashariki kwa wakati huo. Na katika kipindi hicho ni kipindi ambacho taifa la Ujerumani baada ya Berlin conference liliamua kufanya mgawanyo wa bara la afrika na eneo la Afrika mashariki ikiwemo Tanganyika, Rwanda na Burundi lilikuwa koloni la Wajerumani."

Chifu Emmanuel Xavier Zulu Gama wa kwanza ni kiongozi wa jamii wa wangoni kutoka songea Tanzania. Yeye amefika hapa Berlin ili kushuhudia baadhi ya vitu vilivyoibwa kutoka jamii yake.

"Kitu kikubwa sana kinachoeleweka ni mkuki wenye mamlaka. Lakini vilevile kuna kitu kinaitwa koza, koza ni kama bangili ambayo imetengenezwa kwa pembe ya ndovu, ukiunganisha vyote viwili ndio unapata mamlaka kamili ya Chifu pale."

Soma:Pambana! Jinsi Waafrika Mashariki walivyokabiliana na ukandamizaji wa kikoloni

Chifu Mkwawa anajulikana sana katika historia ya Tanzania. Alikuwa kiongozi mkuu wa kabila la Wahehe na alikuwa maarufu kwa kuongoza vita vya kabila lake dhidi ya Wajerumani.

Wakoloni wa Kijerumani katika mji wa Tabora

Hii leo kabila hilo bado linaendeleza utamaduni wa kuwa na kiongozi na katika maonyesha haya nimekutana na Mtwa Adam Abdul Sapi Mkwawa wa II ambaye ni kilembwe cha Chifu Mkwawa na kiongozi wa Wahehe.

"Mimi nimekuja huku Ujerumani kuwakilisha na kuhakikisha kuwa tulichokuwa tukikiongea na hawa wenzetu wa huku Ujerumani baada ya kututafuta na kutueleza kwamba kuna kifaa cha wazee wetu kilichukuliwa, ambacho tulikuwa tunafahamu lakini hatujui kiko maeneo gani. Sasa mimi kama kiongozi na mwakilishi wa kabila la Wahehe imenibidi nifike huku nikiangalie hicho chombo, nihakikishe kwamba ni chombo cha kwetu na kilikuwa chombo cha babu yetu."

Makumbusho ya Ethnolojia ya Berlin kwa sasa yanahifadhi zaidi ya "vitu" 10,000 vilivyotokea Tanzania. Zaidi ya 80% ya mali hizi za kitamaduni zilichukuliwa wakati wa utawala wa kijerumani na Uingereza. Maike Schimanowski ni mhifadhi kutoka Berlin, nilimuuliza mchakato wa kurejesha mali hizi umefikia wapi? "Maonyesho haya yameandaliwa mahsusi na yatapelekwa Dar es salaam na vitu kuonyeshwa kwa umma na havitorudishwa Ujerumani"

Soma kwa kina: Mipaka inayoudhi: Kwa nini Afrika bado inapigania mipaka ya wakoloni?

Maonyesho haya yamewashirikisha wasanii tofauti wa uchoraji, filamu, dansi, picha na muziki. Baada ya onesho la Berlin maonyesho hayo yatafanyika katika makumbusho ya taifa Tanzania huku maandalizi yakifanyika ili kuzirejesha mali hizo kwa jamii za kitanzania.