1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano makali yazuka Burundi

Saumu Mwasimba4 Septemba 2007

Hali ya wasiwasi imewakumba wakaazi wa eneo la Buterere kaskazini mwa mji mkuu Bujumbura baada ya kuzuka mapigano makali kati ya makundi mawili ya waasi wa FNL yanayotofautina.

https://p.dw.com/p/CB1X
Imeripotiwa kiasi cha watu 5000 wamekimbia makazi yao Buterere
Imeripotiwa kiasi cha watu 5000 wamekimbia makazi yao ButererePicha: AP

Watu zaidi ya 21 wameuwawa kwenye mapigano hayo.

Mapigano ya leo ndio mabaya kabisa kuwahi kushuhudiwa katika mji mkuu wa Burundi Bujumbura katika kipindi cha miaka 2 hali ambayo imezusha upya hofu kwamba mkwamo wa kisiasa na juhudi za amani huenda zikaibua mapigano mengine ya wenyewe kwa wenyewe katika nchi hiyo ndogo ya afrika ya kati.

Afisa wa polisi Anaclet Nindabire ameliambia shirika la habari la AFP kwamba maiti 21 zilipatikana katika eneo la kaskazini la Buterere ambako mapigano yaliibuka usiku.

Meya wa Bujumbura Elias Buregure alieleza kuwa mapigano hayo yaliyodumu kwa muda wa saa moja yalizuka kati ya makundi mawili ya FNL yanayotafautiana.Mojawapo ya makundi hayo linampinga Agaton Rwasa kuwa kiongozi wa FNL.

Kiasi cha wafuasi 200 wanampinga bwana Rwasa wakisema hawamtambui tena kuwa kiongozi wao.

Kufuatia mapigano hayo raia 5000 asubuhi ya leo walionekana wakiyahama makazi yao.

Duru za kijeshi mjini Bujumbura zilifahamisha kwamba mapigano ya leo yalianza baada ya kundi moja la FNL linalompinga Rwasa lililoko katika eneo la Buterere kuvamiwa na vikosi vya kundi jingine la FNL linalomuunga mkono Agaton Rwasa.Kundi la waasi wakihutu FNL ni kundi pekee kati ya makundi saba ya waasi Burundi ambalo halijakubali kutia saini makubaliano ya amani na serikali.Viongozi wa kundi hilo waliokuwa wakishiriki mazungumzo ya utekelezwaji wa makubaliano ya amani walijitoa katika mazungumzo hayo na kutoweka mwezi July na kurejea msituni hali iliyoibua wasiwasi wa kuzuka ghasia mpya nchini Burundi.

Kundi hilo la FNL na serikali ya rais Pirre Nkurunzinza zilifikia makubaliano ya kukomesha mapigano mwezi Septemba mwaka 2006 lakini utekelezwaji wa makubaliano hayo limekuwa suala linalozusha ubishi.

FNL linaishutumu serikali kwa kukataa kuviondoa vikosi vyake katika maeneo wanayoyadhibiti na kutaka pafanyike mazungumzo zaidi kuhusu majukumu watakayochukua watakapojumuishwa katika jeshi jipya la serikali na polisi.

Rais wa Burundi na kiongozi wa waasi wa FNL Agaton Rwasa wanatarajiwa kukutana nchini Tanzania katika kipindi cha siku kadhaa zijazo katika sehemu ya mkutano wa kilele wa eneo hilo ambao utahudhuriwa pia na nchi jirani pamoja na mpatanishi Afrika Kusini.

Itakumbukwa kwamba hivi karibuni shirika la kimataifa linashughulikia masuala ya mizozo lenye makao yake mjini Brussels ICG lilitoa ripoti yake iliyotoa wito kwa mataifa ya kigeni kusaidia katika kuyakwamua mazungumzo ya amani nchini Burundi.

Mbali ya kukwama kwa mazungumzo hayo ya kutafuta amani,Burundi pia imekuwa kwenye mzozo wa kisiasa kwa miezi kadhaa sasa mivutano ndani ya chama tawala cha CNDDFDD ambayo imemsababishia rais kukosa wingi wa viti bungeni huku baadhi ya wapinzani wakimshutumu kwa kushindwa kuiongoza nchi.