1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yaripuka Burundi

Oummilkheir4 Septemba 2007

Waasi wanaohasimiana wa kundi la FNL wapigania madaraka ya ndani

https://p.dw.com/p/CH8Y
Rais mpya wa Burundi Pierre Nkurunziza
Rais mpya wa Burundi Pierre NkurunzizaPicha: AP

Mapigano yameripuka mapema leo asubuhi kati ya makundi mawili yanayohasimiana ya waasi wa “Forces Nationales de Libération-FNL nchini Burundi.Waasi sita wameuwawa na watu wanayapa kisogo maskani yao.

Mapigano hayo yameripuka kaskazini mwa mji mkuu Bujumbura.

“Nimewaona watu wengi wakiyapa kisogo maskani yao,wanasema wanakimbia kwasababu makundi mawili hasimu ya FNL yanapigana Butere”amesema hayo Prosper Nzeyimana,mkaazi wa Cibitoke,eneo lililoko karibu sana na mahala mapigano yanakotokea.

Amesema milio ya risasi na mizinga ndio iliyomzindua toka usingizini.

Msemaji wa jeshi la Burundi,Adolphe MANIRAKIZA amethibitisha ripoti kuhusu mapigano kati ya makundi hayo mawili ya FNL yalihusu uongozi wa Agathon Rwasa.Makundi yote hayo mawili hasimu yamepiga kambi katika vitongoji vya Kinama na Buterere,kaskazini mwa mji mkuu Bujumbura.

“Mapigano ni kati ya waasi wanaompinga Agathon Rwasa kama mwenyekiti wa Forces Nationales de Libération FNL na wale wanaomuunga mkono”-amesema hayo Adolphe MANIRAKIZA mbele ya maripota wa shirika la habari la Uengereza Reuters.

Makundi haya mawili yalipigana pia jumapili iliyopita lakini mapigano hayo hayakua makali kama leo.

Mashahidi wanasema waasi sita wameuwawa kufuatia mapigano hayo.”Nimeona maiti sita njiani,pengine wengi zaidi wameuliwa” amesema shahidi mmoja ambae hakutaka jina lake litajwe.

Kundi la FNL ni kundi pekee la waasi wa kihutu wanaoendelea kupigana nchini Burundi-ambako vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoripuka mwaka 1993 vimeshagharimu maisha ya zaidi ya watu laki tatu.

Makubaliano yalifikiwa mwezi June uliopita kati ya serikali ya Burundi na kundi hilo la waasi wa kihutu ili kutia njiani makubaliano ya amani yaliyotiwa saini mwaka 2006.Lakini mwezi uliopita FNL walijitoa katika tume ya pamoja ya kusimamia makubaliano ya kuweka chini silaha.

Mwishoni mwa mwezi uliopita Umoja wa Afrika uliwasihi waasi wa FNL warejee katika tume hiyo ili kuunusuru utaratibu wa amani.

Akizungumza na waandishi habari mpatanishi wa Afrika kusini katika mzozo wa Burundi Charles Nqakula amesema tunanukuu:

“Tumepewa jukumu na Umoja wa Afrika kuendeleza vyema shughuli zetu hadi ifikapo december 31 ijayo ,ikimaanisha FNL na wote wengine wanabidi warejee katika tume ya pamoja ya kusimamia makubaliano ya kuweka chini silaha.”Mwisho wa kumnukuu mpatanishi huyo wa kutoka Afrika kusini.

Waasi wanadai wako tayari kujiunga upya na tume hiyo ikiwa usalama wao utadhaminiwa.